GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU

- 8 -

Kwa Nini Kifo cha Yesu ni Muhimu?

Kwa sababu mwanadamu hawezi kujiokoa mwenyewe, ni Mungu tu anayeweza kuutengeneza wokovu kwa ajili ya mwanadamu. Tumeona kwamba tunaokolewa kwa sababu ya neema ya Mungu, kwa njia ya imani katika kifo na ufufuo wa Bwana Yesu kama malipo ya dhambi zetu zote. Bwana Yesu alifanya kazi kubwa kwa ajili yetu alipokufa msalabani. Tutaona hapo chini jinsi kifo chake kilivyoutengeneza wokovu wetu. Ni kwa sababu hiyo kifo cha Yesu ni muhimu.
 
A. Kifo Cha Yesu ni Muhimu kwa Sababu Yesu Asiye na Dhambi Aliweza Kufa Badala ya Wanadamu Akiadhibiwa kwa Ajili ya Dhambi Zao Zote.

Ni lazima mwanadamu asiye na dhambi afe kwa ajili ya mwanadamu mwenye dhambi.

Tulishaona kwamba Mungu aliye mwenye haki analazimika kuadhibu dhambi zote. Ili tuweze kuokolewa tunahitaji kukwepa adhabu ya dhambi zetu. Tuliona hali hii inawezekana tu ikiwa mwingine ataadhibiwa badala yetu. Kama mwingine anaweza kulipa deni letu Mungu ataacha hasira yake na tutakuwa tumepatanishwa na kurejezwa katika ushirika wetu naye. Yaani, tutakuwa tumeokolewa.

Nani anaweza kuadhibiwa badala yetu? Biblia inasema ni lazima mwanadamu aadhibiwe kwa ajili ya dhambi za wanadamu (Ebr 2:14-17). Mungu hatapokea kifo cha mnyama kama malipo ya dhambi za wanadamu (Ebr 10:4) na hata malaika hawawezi kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi za wanadamu.

Pili, yule atakayeadhibiwa badala ya wanadamu wenyewe, lazima asiwe na dhambi. Mwanadamu mwenye dhambi hawezi kuadhibiwa kwa ajili ya mwingine. Mwenye dhambi ni lazima aadhibiwe kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. Tumeshaona adhabu ya dhambi, hata moja, ni adhabu ya milele. Kutokana na hali hii, mwenye dhambi hawezi kumaliza adhabu yake ili aadhibiwe kwa ajili ya mtu mwingine mwenye dhambi. Hivyo, ili mtu mwingine aadhibiwe kwa ajili ya dhambi zetu, inabidi yule mwingine awe mwanadamu asiye na dhambi; yaani mtu ambaye amemtii Mungu asilimia mia bila kuvunja hata amri au agizo moja.

Yesu aliweza kufa kwa ajili yetu kwa sababu alikuwa mwanadamu 100% asiye na dhambi

Ni mtu gani anayeweza kufanya hivyo? Mwenye sifa hiyo? Hakuna! Biblia inasema “wote wametenda dhambi” (Rum 3:23).

Hapo tunaona ukuu wa neema ya Mungu na sababu tunaweza kuokolewa kwa neema yake tu. Kwa kuwa hakuna mtu anayeweza kuadhibiwa kwa ajili ya mwandamu mwenzake kutokana na hali ya wote kuwa wenye dhambi wanaostahili hukumu, Mungu alimtuma Mwana wake azaliwe hapa duniani. Mwana wa Mungu alizaliwa kama mwanadamu (Gal 4:4) na aliitwa Yesu. Kwa sababu Yesu alikuwa Mungu pia, aliweza kuishi bila kutenda dhambi hata moja (2 Kor 5:21). Pia kwa sababu Yesu hakuwa na dhambi yo yote (Ebr 4:15), yeye pekee aliweza kuzichukua dhambi za ulimwengu na kuadhibiwa badala yetu. Kristo alipokufa, alizichukua dhambi zetu zote. Aliadhibiwa badala yetu sisi ili tusiadhibiwe kamwe (Isa 53:5,6; 2 Kor 5:21; 1 Pet 2:24).

Kwa kuwa Yesu ni 100% Mungu aliweza kufa kwa ajili ya dhambi za wanadamu wote.

Lakini tukumbuke kwamba wakati Yesu alipokufa alikuwa asilimia mia moja mwanadamu na asilimia mia moja Mungu wakati mmoja. Kwa kuwa alikuwa mwanadamu aliweza kufa kwa ajili ya wanadamu wenzake. Lakini ni muhimu pia kwamba Yesu alikuwa Mungu wakati alipofia dhambi za wanadamu wote. Kifo cha mwanadamu mmoja wa kawaida kisingeweza kubeba dhambi za wanadamu wote. Mwanadamu wa kawaida asiye na dhambi angeweza kuadhibiwa kwa ajili ya mwanadamu mwenye dhambi mmoja tu. Tukumbuke mshahara au adhabu ya dhambi ni mauti ya milele. Hivyo mtu huyu mmoja wa kawaida angehitaji kuadhibiwa milele kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja, ili mwenye dhambi asiadhibiwe. Na kwa njia hii huyu asiye na dhambi asingeweza kumaliza adhabu hiyo ili aadhibiwe kwa ajili ya wengine pia.

Lakini, kwa sababu Yesu alikuwa asilimia mia Mungu, umungu wake ulimwezesha kufia dhambi za watu wote. Uwezo huo unatokana na thamani ya kifo chake; yaani kifo cha Mungu.

Tena umungu wa Yesu ulimwezesha Yesu kuadhibiwa kwa muda mfupi badala ya hitaji la kuadhibiwa milele.
 
B. Kifo cha Yesu ni Muhimu kwa Sababu Ghadhabu ya Mungu Juu ya Wenye Dhambi Ilitulizwa Wakati Yesu Aliadhibiwa Badala ya Wenye Dhambi Wenyewe

Mungu aliitoa ghadhabu yake juu ya Yesu

Sisi wenye dhambi tulikuwa chini ya ghadhabu ya Mungu. Kristo alipoipokea adhabu ambayo sisi tulistahili kuipokea, ghadhabu ya Mungu ilimwagika juu ya Yesu. Ndiyo sababu wale wanaomwamini Kristo hawatapokea ghadhabu ya Mungu tena. Kwa sababu ghadhabu ya Mungu imetulizwa msalabani, njia ya sisi kupatanishwa na Mungu ilifunguliwa.
 
C. Kifo Cha Yesu ni Muhimu kwa Sababu Kupitia Kifo Hicho Kristo Alimshinda Shetani Ili Aweze Kutukomboa Tusiwe Chini ya Mamlaka ya Shetani Tena.

Sisi wenye dhambi tulikuwa chini ya mamlaka ya Shetani. Yesu alimshinda Shetani ili tuwe huru kutoka chini ya mamlaka ya Shetani (Ebr 2:14-15). Sasa, tuko chini ya utawala wa Mungu; Muumba wetu anayetupenda (Kol 1:13).
 
D. Kifo cha Yesu ni Muhimu kwa Kuwa Katika Kifo Chake Utu Wetu wa Kale Ulikufa Ili Tukombolewe na Utumwa wa Dhambi.

Sisi wenye dhambi tulikuwa tunatawaliwa na utu wa kale na tulikuwa watumwa wa dhambi. Ndiyo kusema kielelezo cha maisha yetu kilikuwa kutenda dhambi kwa kuwa kama mtumwa wa dhambi hatukuweza kutotenda dhambi. Yesu aliposulubishwa, utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye. Maana ya kufa kwa utu wa kale ni kusema tuliondolewa kutoka kuwa chini ya utawala wa utu wa kale au dhambi katika maisha yetu (Rum 6:6-7). Mabadiliko hayo yana maana aliyemwamini Yesu siyo mtumwa wa dhambi tena na nguvu za Shetani zimevunjwa. Kama wakristo, bado tuna uwezo wa kutenda dhambi, lakini kuna uchaguzi sasa. Tunaweza kuchagua kutenda dhambi au kutotenda kwa kuwa sisi hatujawa watumwa tena wa dhambi.

Tumeona ni kweli Yesu aliifanya kazi kubwa kwa ajili yetu alipokufa msalabani. Aliipokea adhabu ya dhambi zetu ili atupatanishe na Mungu na kutukomboa kutoka kwa Shetani, na dhambi. Kifo chake kilitosha kutuokoa. Tusichoke kumshukuru Mungu kwa kazi yake kuu!


RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 9
Proudly powered by Weebly