GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU

- 5 -

Basi, Tuna Tumaini Lo lote la Kuokolewa?

Tumeona kwamba sisi ni wafu kiroho na hatuwezi kujisaidia mbele ya Mungu. Tumeona kwamba Mungu ni mtakatifu na mwenye haki na hivyo hatashirikiana na mtu asiye mtakatifu, bali ataziadhibu dhambi zake. Basi, tuna tumaini lo lote la kuokolewa? Ndiyo!

Tumaini = Upendo, Rehema, na Neema ya Mungu

Tuna tumaini kwa sababu Mungu ni mwema. Tunamaanisha nini tunaposema kwamba Mungu ni mwema? Wema wa Mungu unaonekana kwa njia tatu. Njia hizi ni kupitia upendo wake, rehema yake, na neema yake. Upendo ni kumtakia mwingine wema katika maisha yake. Rehema ni kutowaadhibu wanaostahili adhabu. Neema ni kumtendea mtu kwa wema wakati anastahili kuadhibiwa.

Tunaposema kwamba Mungu ni mwema, tunasema kwamba Mungu katika upendo wake anataka kututendea vizuri. Katika rehema yake, hataki kutuadhibu. Katika neema yake, anataka kutusaidia ingawa tunastahili kuadhibiwa.

Upendo wa Mungu

Yohana 3:16 – “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Upendo ni kumtakia mtu mwingine wema katika maisha yake, yaani mambo mazuri. Kwa mfano, Linus alifika shuleni lakini alikuwa amesahau daftari lake na mwalimu wake alimlazimisha kurudi nyumbani. Lakini Yakobo, rafiki wa Linus, hakutaka Linus arudishwe nyumbani. Hivyo Yakobo alimpa Linus daftari lake la akiba. Nia ya Yakobo kumsaidia Linus ilitokana na upendo wake kwa Linus. Kama tunavyoona katika mfano huu, upendo huoneshwa kupitia matendo.

Tunaposema Mungu ni pendo, tunamaanisha Mungu ana nia njema kwetu na anatutakia wema katika maisha yetu. Kutokana na msimamo huo anatuonesha upendo wake kupitia matendo yake.
  
Rehema ya Mungu

Rehema ni kutoadhibu mtu anayestahili kuadhibiwa. Kwa mfano siku moja mtoto anayeitwa Antonio alivunja kikombe cha baba yake wakati baba yake alikuwa shambani. Wakubwa wa Antonio walimwambia, “Baba atakaporudi tutamwambia na yeye atakupiga!” Antonio aliogopa kupigwa na babaye. Baba yake aliporudi, Antonio hakuenda kumsalimia pamoja na wakubwa wake. Wakubwa wake walimwambia baba yao jinsi Antonio alivyovunja kikombe kile. Baba yake, kwa hasira, alimwita Antonio aje. Antonio alianza kulia na akamwendea baba yake akikiri na kueleza jinsi alivyokosea. Mwishoni, baba yake akamhurumia na hakumpiga ingawa alistahili kuadhibiwa.

Tunaposema Mungu ni mwenye rehema tunamaanisha jinsi Mungu hataki tuadhibiwe na jinsi anavyotafuta njia kutusaidia kukwepa adhabu yake iliyo ya lazima. Ukweli ni kwamba tunapofanya kosa lo lote, siku ile ile Mungu angeweza kutuhukumu milele. Lakini Biblia inasema kawaida Mungu hatoi adhabu siku ile ile, bali anatuvumilia kutokana na wema na rehema yake (Rum 2:4). Anataka tupewe nafasi ya kutubu na kukubali wokovu wake ulio njia pekee ya kukwepa adhabu tunayostahili.

Neema ya Mungu

Waefeso 2:8 – “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu”

Neema ni kumtendea mema mtu mwingine asiyestahili kutendewa mema. Kwa mfano mgonjwa aliye na vidonda kwenye miguu yake alienda kumwona daktari ili atibiwe. Daktari huyu alitibu na kufunga miguu ya mgonjwa huyo. Mgonjwa alipoondoka, aliona kaptura za daktari huyu zimeanikwa nje, akaziiba na kuondoka nazo. Kwa bahati, daktari huyu akawa ameona tendo hilo dirishani. Kesho yake mgonjwa huyu alirudi kutibiwa tena. Je, alistahili msaada wa daktari huyu? Hapana. Lakini daktari huyu aliendelea kumtibu ingawa mgonjwa huyu hakustahili wema wake. Badala yake alistahili adhabu. Daktari huyu alipoendelea kumtibu bila kuita polisi, alikuwa akimwonesha neema mgonjwa huyu.

Tunapoongea kuhusu neema ya Mungu tunaongea kuhusu hali yake ya kututendea mema wakati tunastahili adhabu.

Hali hizo zote za Mungu, wema, upendo, rehema, na neema, zinafanya kazi ili mtu aokolewe. Tunaona hali hizo zote katika Waefeso 2:1-9 inayoongea jinsi tulivyopotea, jinsi tulivyokuwa chini ya hasira ya Mungu, na jinsi wema, upendo, rehema, na neema ya Mungu zilivyotupa tumaini la kuokolewa.

Waefeso 2:1-9 – “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa REHEMA, kwa mapenzi yake makuu aliyotuPENDA; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa NEEMA. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa NEEMA yake upitao kiasi kwa WEMA wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa NEEMA, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

Kwa sababu Mungu ni mwema, pendo, mwenye neema na rehema, anatujali na anataka tusiadhibiwe kwa ajili ya dhambi zetu. Lakini Mungu ni hakimu mwenye haki vilevile. Kwa sababu hiyo analazimika kuhukumu na kutoa adhabu kwa mwenye dhambi. Akifuta adhabu yao tu, atakuwa hajatenda haki – hali isiyowezekana kwa Mungu.

Mfano wa Petro, Esau, na Hakimu

Unakumbuka hadithi ya Petro na Esau? Hadithi hiyo inaweza kutuonesha namna Mungu anavyoweza kutuhurumia, na wakati huo huo, aziadhibu dhambi zetu. Tukumbuke kwamba hakimu aliamua kwamba Esau aliiba ng’ombe na alipaswa kulipa 70,000/= kama adhabu yake. Esau aliomba ahurumiwe kwa sababu ya shida ya mkewe. Je, hakimu angeweza kumhurumia Esau asilipe adhabu hiyo na wakati huo huo atende haki? Jibu ni ndiyo. Tuone jinsi hakimu alivyoweza kumhurumia Esau na kuhakikisha adhabu yake ilipwe. Kwanza, Hakimu alijua hawezi kumwacha Esau aende zake bila adhabu yake kulipwa. Kwa sababu ya huruma yake, hakimu alikubali kumlipia adhabu yake. Alitoa pesa kwenye mfuko wake na akampa Esau ili Esau alipe deni la adhabu yake. Kwa njia hii, wizi wa Esau uliadhibiwa na Esau alihurumiwa. Esau aliondoka akiwa na shukrani na furaha sana kwa sababu alikubali kuupokea msaada wa hakimu huyu.

Je, hakimu angekubali Esau asilipe adhabu yake, angekuwa ametenda haki? Hapana, kwa sababu uovu wa Esau usingeadhibiwa. Je, hakimu alipoilipia adhabu ya wizi ya Esau, alitenda haki? Ndiyo, kwa sababu uovu wa Esau uliadhibiwa. Kupitia upendo, neema, na huruma ya hakimu, adhabu ya Esau ililipwa bila Esau binafsi kuadhibiwa.

Katika mfano huu, adhabu ya Esau ililipwaje bila Esau kuadhibiwa? Adhabu ya Esau ililipwa wakati mwingine alikubali kubeba gharama ya Esau – yaani kwa namna nyingine hakimu aliadhibiwa badala ya Esau.

Kuna njia peke gani ambayo Mungu anaweza kutuhurumia tusiadhibiwe na wakati huo huo gharama ya adhabu yetu ilipwe? Kwa njia ya Mungu kumwadhibu mwingine badala yetu. Wakati Mungu anamwadhibu mwingine kwa ajili ya dhambi zetu, adhabu inalipwa, haki inatendeka, na sisi wenyewe hatuhitaji kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zetu.
Wokovu wa kibiblia ni jibu la Mungu kuadhibu dhambi zetu bila sisi wenyewe kuadhibiwa kwa kuwa anaadhibu mwingine badala yetu.
​
Kwa nini tuna tumaini la kuokolewa?

Ingawa sisi ni wenye dhambi wasio na tumaini la kujiokoa, bado tuna tumaini la kuokolewa kwa sababu Mungu ni mwema na ametengeneza njia ya kuadhibu dhambi zetu bila kutuadhibu sisi wenyewe kwa kuadhibu mwingine badala yetu. Hili ndilo tumaini pekee tulilo nalo.

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 6
Proudly powered by Weebly