GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU

- 4 -

Kwa Nini Sheria Haiwezi Kutuokoa?

Watu wengine wanadhani Mungu alitoa sheria yake ili watu waokolewe kwa kuitii. Lakini hii siyo sababu ya Mungu kutoa sheria yake. Sheria haina uwezo wa kuokoa. Tuone kwa nini sheria haiwezi kuokoa.

Sheria ya Mungu ni kipimo kamili ambacho Mungu atumia kupima wema wa watu. Sheria inaonesha mtu jinsi anavyopaswa kuishi ili akubaliwe na Mungu. Ili mtu akubaliwe na Mungu kupitia sheria, mtu huyu atalazimika kutimiza sheria zote za Mungu wakati wote. Lakini, hakuna mtu anayeweza kufanya hivyo. Kuanzia Adamu hadi leo, hakuna mwandamu, hata mmoja, aliyetimiza kikamili sheria ya Mungu isipokuwa Yesu Kristo tu.
 
A. Sheria Ina Kusudi Gani Basi?

Kama wanadamu hawawezi kujiokoa kwa kutii sheria, je, kwa nini Mungu alitoa sheria yake? Tutaona kwa nini Mungu aliwafahamisha wanadamu sheria zake kwa kusoma maelezo ya Mungu katika Biblia.

Kusudi la sheria ni kuonesha dhambi iwe wazi

Warumi 3:20 – “Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.”

Warumi 7:7 – “Tusemeje, basi? Torati (torati ni sheria) ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani”.

Sheria haina kusudi la kuondoa dhambi, bali kuonesha dhambi ilipo. Kwa kawaida asiye Mkristo hajui yeye ni mwenye dhambi mbele za Mungu. Kazi ya sheria ni kumwonesha mtu kama huyu kwamba yeye kweli ni mwenye dhambi kwa kuwa matendo yake ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Kusudi la sheria ni kunyamazisha watu mbele ya Mungu ili wasiweze kujitetea

Warumi 3:19 - “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu”

Watu wengine wanadhani kwamba katika siku ya hukumu watamwomba Mungu awahurumie kwa sababu hawakufanya dhambi zilizo mbaya sana au kwa sababu matendo yao mema yalizidi matendo yao mabaya. Lakini watu hawa wamekosea katika mawazo yao kwa sababu Warumi 3:19 inadai hawataweza kujitetea; yaani hata kufungua kinywa chao hawatafanya. Sababu ni kwamba sheria itaonesha dhambi zao zote. Watajiona wenye hatia kweli kweli na wataona hakuna haja kujaribu kujitetea.

Kusudi la sheria ni kuleta ghadhabu ya Mungu

Warumi 4:15 – “Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.”

Zaidi ya kuwa chini ya hukumu tu, wote wanaovunja sheria za Mungu wako chini ya ghadhabu yake vilevile. Wote walio chini ya ghadhabu ya Mungu watatupwa katika ziwa la moto.

Kusudi la sheria ni kuhukumu

Warumi 2:12 – “Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria.”

Yakobo 2:10 – “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.”

Ye yote atakayeweza kutimiza sheria zote za Mungu atahesabika kuwa haki mbele ya Mungu. Lakini wale wanaofanya hata kosa moja watahukumiwa na sheria hiyo. Hukumu ya kutotii sheria, hata moja, ni nini? Ni mauti ya milele. Sheria inatuhukumu sisi sote kwa sababu hakuna hata mwanadamu mmoja kati yetu anayeweza kutii kila sheria ya Mungu kila wakati.

Sheria ya Mungu inalaani

Wagalatia 3:10 – “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.”

Sheria ya Mungu inaleta ghadhabu na hukumu, lakini pia inaleta laana kwa wote watakaoshindwa kutimiza sheria zote kikamili. Je, laana ya sheria ni nini? Laana ya sheria ni mauti.

Sheria inaua

2 Wakorintho 3:6 – “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.”

Sheria inaua kwa kuwa ye yote atakayevunja hata sheria moja anahukumiwa na mauti ya milele. Ina maana sheria inatuhukumu sisi sote kufa kwa kuwa wote tumevunja angalau sheria moja (Rum 3:23).

Sheria inatuongoza kwa Kristo

Wagalatia 3:23-24 – “Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.”

Mungu anasema wazi katika Wagalatia 3:23-24 kwamba alitoa sheria yake ili itumike kama chombo cha kuleta watu kwa Kristo.

Tuseme, kwa mfano, una shida na anayeweza kukusaidia ni Mkuu wa Mkoa. Unafanya safari ya kwenda mkoani lakini hujui Mkuu wa Mkoa anakaa wapi. Ukipata mtu wa kukuongoza hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa, je, mtu huyu ana uwezo wa kutatua shida yako? Hapana. Kazi yake ni kukuonesha mahali pa yule anayeweza kukusaida. Baada ya kukuonesha mahali Mkuu wa Mkoa alipo, kazi yake imeisha.

Hii ndiyo kazi ya sheria ya Mungu. Sheria ya Mungu haiwezi kutusaidia na shida yetu ya dhambi. Yaani, haiwezi kutuokoa. Lakini kazi yake ni kutuongoza. Kwanza inatuongoza kuelewa na kukubali shida ya dhambi tuliyo nayo. Bila kutambua tunayo shida, hatuwezi kutafuta tiba ya shida hiyo. Pili inatuongoza kwa Yesu Kristo kwa kuwa yeye ndiye mwenye jibu la shida yetu. Tukishachoka katika kujaribu kujiokoa kupitia sheria, tutakuwa tayari kupokea zawadi ya Mungu kumpitia Yesu Kristo.
 
B. Mambo Ambayo Sheria Haiwezi Kuyafanya


  • Sheria ya Mungu haiwezi kutuhesabu haki mbele ya Mungu (Rum 3:21, 9:30-33, Gal 2:15-16).
  • Sheria haiwezi kuondoa dhambi (Heb 10:1-4).
  • Sheria haiwezi kumfanya mtu awe hai (Gal 3:21).
  • Sheria haiwezi kuokoa (Rum 8:3).

Katika mistari hii pamoja na mingine, Biblia ni wazi kwamba hakuna anayeweza kuokolewa kwa njia ya kutii sheria ya Mungu.

​Kwa nini sheria haiwezi kutuokoa?


Sheria inaweza kuokoa tu wale wanaoweza kutii sheria ya Mungu asilimia mia. Wote wanaovunja hata sheria moja wanahukumiwa na sheria hiyo. Kwa sababu tunazaliwa na asili ya dhambi hatuwezi kutii sheria zote za Mungu bila kukosea angalau mara kwa mara. Kwa sababu hiyo, sheria inatuhukumu tu. Haiwezi kutuhesabu haki wala kutuokoa kwa sababu inatangaza sisi ni wavunja sheria. Ndiyo maana Biblia inasema katika Warumi 8:2-3, “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili…” Shida siyo sheria ya Mungu. Sheria ya Mungu ni “haki”, “takatifu”, na “njema” (Rum 7:12). Ila shida ni udhaifu wa wanadamu na jinsi wasivyoweza kutii sheria ya Mungu kikamilifu.
 
 Kuna mifano miwili hapo chini. Mifano hii inaonesha kwa nini sheria haiwezi kutuokoa.

Mfano #1 – Gereza la nchi fulani duniani 
Picture
​Picha hii inaonesha mtu ambaye hajavunja sheria yo yote katika nchi yake. Hivyo ni mwenye haki na anakaa huru nje ya gereza.
Picture
​Picha hii inaonesha jinsi mtu huyu alivyoiba mbuzi wa mwingine, akakamatwa, na hakimu alimhukumu akae gerezani mwezi mmoja kama adhabu yake.
Picture
Baada ya mwezi mmoja kutimia mtu huyu alimaliza adhabu yake. Kumaliza adhabu yake kunamfanya ahesabike tena kuwa mwenye haki; yaani hana hatia sasa. Hivyo anaachwa huru nje ya gereza tena.
 
Mfano #2 – Gereza la Mungu la milele
Picture
​Katika picha hii, mtu huyu yuko huru kwa kuwa hajavunja sheria yo yote ya Mungu. Maana yake ana uhusiano mzuri na Mungu na anapokelewa na Mungu.
Picture
Katika picha hii, mtu huyu alitenda dhambi moja. Aliiba mbuzi wa mwingine na Mungu mwenye maarifa yote aliona na kujua kuhusu dhambi hiyo. Mwisho, Mungu kama hakimu alimhukumu mtu huyu kulingana na sheria na kanuni yake. Kutokana na dhambi yake, na kulingana na udhaifu wake kama mwanadamu mwenye dhambi, mtu huyu analazimika kukaa gerezani milele kwa kuwa adhabu yake ni kubwa mno. Hawezi kumaliza deni lake, hivyo ataendelea kukaa gerezani na kuendelea kulipa milele.
​
Mtu huyu atatoka gerezani lini? Kamwe – yaani, hatatoka tena. Kwa nini? Kwa sababu hawezi kumaliza adhabu yake. Kwa kuwa adhabu ya kuvunja hata sheria moja ndogo ya Mungu ni mauti ya milele, ni lazima mtu huyu aadhibiwe milele. Ndiyo maana sheria haiwezi kuokoa. Hakuna anayeweza kutii kila sheria ya Mungu kila wakati. Hivyo sheria inamhukumu kila mtu kwa kuwa inaonesha mahali alipokosea mapenzi ya Mungu. 

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 5
Proudly powered by Weebly