GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU

- 1 -

Habari ya Wokovu Ulianzaje?

Ujumbe wa wokovu unaanza na Mungu. Ni muhimu tuanze na Mungu kwa sababu wale wanaotaka kuokolewa lazima waamue kama wanataka kuwa na uhusiano na Mungu wakimwabudu au la.

Mstari wa kwanza wa Biblia unaanza kwa kusema, “Hapo mwanzo…” (Mwa 1:1). Tunajifunza kutoka maneno haya mawili kwamba kila kitu kina mwanzo wake. Vitu vinavyoonekana na hata vitu visivyoonekana vilikuwa na mwanzo. Kabla ya mwanzo huo hapakuwa mbingu, wala dunia, wala cho chote katika dunia. Watu wanahitaji vitu katika dunia hii ili waishi, kwa hiyo, hata watu hawakuwepo wakati hapakuwa dunia. Vizazi vilivyotutangulia havikuwepo wakati huo kabla ya mwanzo na hata malaika na pepo hawakuwepo.

Mwanzo 1:1 unaendelea ukisema, “Hapo mwanzo Mungu…” Hapo mwanzoni, wakati Mungu bado hajaumba kitu, wakati hapakuwa watu wala viumbe vya roho, kitu kimoja tu kilikuwepo. Yaani Mungu peke yake alikuwepo. Biblia ni wazi kwamba Mungu alikaa peke yake kabla ya mwanzo. Hapakuwapo hata miungu mingine. Biblia inafundisha kuhusu Mungu kwamba kuna Mungu mmoja tu (Kum 6:4). Mungu anasema katika Isaya 45:5, “Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu!” Miungu yote mingine ya watu wengine ni sanamu tu na siyo miungu ya kweli (Zab 96:5).

Tukiendelea kusoma Mwanzo 1:1 tunaona yale Mungu aliyoyafanya hapo mwanzo: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Jambo la pili tunalojifunza kuhusu Mungu ni kwamba yeye ndiye mwumbaji wa vitu vyote. Wakati Mungu alipoumba mbingu, aliumba vilevile vitu vyote vilivyomo mbinguni. Hapo mwanzo Mungu aliumba hata malaika. Pia Mungu aliumba dunia yetu na kila kitu ndani yake kama vile: wanadamu, wanyama, miti, mito, n.k. (Mwa 1:1-2:3).
Mungu ni mkuu kuliko viumbe vyake vyote (Zab 135:5). Anatawala juu ya vyote alivyoviumba (Zab 103:19), ikiwa ni pamoja na wanadamu, Shetani, malaika, na pepo (tazama mchoro #1).
Picture
Mchoro #1. Mungu anatawala viumbe vyote. Katika mchoro huu utawala wa Mungu ni juu ya vitu vyote vilivyo ndani ya mstatili.

Mungu ni mwenye uweza wote. Ndiyo maana aliweza kuumba vitu vyote (Yer 32:17). Hakuna jambo lisilowezekana kwake Mungu. Aliumba yote aliyoyataka. Mungu ana uwezo na nguvu kuliko viumbe vyake vyote. Hakuna kitu kilichoumbwa chenye nguvu au mamlaka kuliko Mungu. Hata Shetani hana nguvu au mamlaka kuliko Mungu.
​
Kwa nini Mungu aliumba viumbe vyote? Mungu aliumba vitu vyote ili atukuzwe yeye (Isa 43:7a; Zab 148:1-13). Zaidi, Mungu aliwaumba wanadamu na malaika wamtumikie (Kut 20:3-5a; Heb 1:14). Makusudi makuu mawili ya Mungu kuumba wanadamu na malaika ni kumtukuza na kumtumikia Mungu.

Siku moja, malaika mmoja aliyeitwa “Nyota ya Alfajiri” (au Lucifer, yaani Shetani) alikuwa na kiburi na hamu ya kutawala kama Mungu atawalavyo; alitaka kuwa sawa na Mungu. Alifikiri ataweza kumshinda Mungu na kuingilia mamlaka yake. Malaika wengi walimwunga mkono Shetani na kwa pamoja walimwasi Mungu wakimpiga vita. Lakini hawakuweza kumshinda mwenyezi Mungu. Mungu aliwatoa mbinguni wakae sehemu za duniani (Eze 28:14-16). Na pia Mungu aliandaa mahali pa adhabu ya milele kwa ajili ya Shetani na wote watakaomfuata katika kutomtii Mungu; mahali panapoitwa jehanamu.

Kuanzia wakati “Nyota ya Alfajiri” alipomwasi Mungu ndipo alianza kuitwa Shetani. Maana ya jina hilo ni “adui”. Shetani ni adui mkuu wa Mungu. Shetani hampendi Mungu na hapendi yote Mungu anayopenda. Ndiyo maana Shetani hapendi wanadamu kwa sababu Mungu anawapenda. Makusudi ya Shetani ni kupiga vita mapenzi yote ya Mungu hata kuangamiza wanadamu wote wanaopendwa na Mungu.

Tangu Shetani alipomwasi Mungu kumekuwa tawala mbili na falme mbili za kiroho. Mungu ndiye mtawala mkuu na mwenye haki kutawala mambo yote. Shetani ni mtawala mdogo anayetawala wale tu wanaomkubali na kumfuata (tazama mchoro #2). Malaika waliomfuata Shetani katika uasi wake wanaitwa pepo wachafu. Shetani hakuridhika kutawala pepo wake tu bali alitaka kutawala wanadamu pia. Tutaona jinsi alivyotaka kuwatawala katika sehemu inayofuata.

Picture
Mchoro #2. Mungu bado anatawala juu ya vitu vyote. Ndiyo maana vyote vimo ndani ya mstatili wa utawala wake. Shetani alipewa ruhusa kutawala juu ya wale wanaochagua kumfuata badala ya kumfuata Mungu. Mstatili mdogo ni mfano wa utawala wake ulio ndani ya utawala wa Mungu.

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 2
Proudly powered by Weebly