WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU
- 15 -
Wokovu Unaleta Mabadiliko Gani Katika Uhusiano Wetu na Mungu?
Tunapookolewa, uhusiano wetu na Mungu unabadilishwa katika sehemu mbalimbali. Tutaona jinsi tunavyorudishwa chini ya utawala wa Mungu, jinsi tunavyobatizwa katika Mwili wa Kristo, jinsi tunavyounganishwa na Kristo, jinsi tunavyopokea Roho Mtakatifu, tunavyohesabiwa haki, tunavyotakaswa, tunavyofanywa watoto wa Mungu, tunavyosamehewa, na tunavyopokea uzima wa milele.
A. Tunapookolewa, Tunarudishwa Chini ya Utawala wa Mungu.
Kuwa huru na dhambi ni kurudishwa chini ya utawala wa Mungu
Kabla Adamu hajafanya dhambi, alikuwa chini ya utawala wa Mungu. Lakini, alipofanya dhambi, alijiweka chini ya mamlaka ya Shetani. Mungu alipotukomboa kutoka katika mamlaka ya Shetani na dhambi, hakutuacha kujitawala wenyewe. Aliturudisha chini ya utawala wake ili awe mtawala wetu tena.
Wakolosai 1:13 – “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.”
Kuwa huru na utawala wa dhambi siyo kuwa huru kufanya dhambi! Kuwa huru na utawala wa dhambi ni kutokuwa mtumwa wa dhambi tena na kuwa mtumwa wa Mungu (Rum 6:22). Mkristo aliye mtumwa wa Mungu anapaswa kumtii nani? Mungu. Anaweza kuishi vile anavyotaka tu? Hapana. Mtumwa anapaswa kumtii na kuyafanya mapenzi ya mtawala wake. Kwa kuwa Mungu ni mtawala wetu, tunatakiwa kuyafanya mapenzi yake.
Maana ya kurudishwa chini ya utawala wa Mungu: Tendo la Mungu kumweka katika ufalme wake yule anayemwamini Kristo.
Matokeo ya kurudishwa chini ya utawala wa Mungu katika maisha ya Mkristo: Mkristo atamtii Mungu na kuishi maisha yanayolingana na mapenzi ya Mungu kwa sababu anafahamu kwamba anatawaliwa na Mungu.
Swali la Kutafakari: Unaoneshaje kwamba wewe ni mtumwa wa Mungu?
B. Tunapookolewa, Tunabatizwa Katika Mwili wa Kristo.
Mungu anatumia mifano mingi kuonesha hali au mahali pa kila Mkristo. Mfano wa kwanza tuliouona ni kwamba Mkristo ni mtumwa katika ufalme wa Mungu. Mfano mwingine, tutakaoangalia sasa, ni kumwelewa Mkristo kuwa ndani ya “Mwili” wa Kristo. Biblia inafundisha kwamba Bwana Yesu Kristo ni kichwa cha mwili huo (Efe 4:15; 5:23; Kol 1:18). Ndiyo maana mwili huo unaitwa Mwili wa “Kristo”. Kila Mkristo ni sehemu au mshiriki wa Mwili wa Kristo. Hivyo, Mwili wa Kristo ni Wakristo wote kwa pamoja (Rum 12:4-5; 1 Kor 12:12-27; Efe 3:6; 4:25; 5:30).
Kazi za kichwa na mwili
Katika somo hilo kuhusu maana ya Mwili wa Kristo tutaangalia kazi za kichwa na pia kazi za mwili. Sisi Wakristo tunapaswa kufahamu wajibu wetu kama wajumbe wa Mwili wa Kristo kwa kuwa ndiyo sababu moja ya Mungu kutuokoa.
Kazi ya kichwa cha mwili huo ni nini? Kazi ya kichwa ni kuongoza na kuamuru mwili. Kila tendo na kila neno ambalo mwili unafanya na kusema unaongozwa na kichwa. Mkono ukishika kitu, unafanya hivyo kwa sababu umeagizwa na kichwa kufanya hivyo. Yesu Kristo anaitwa Bwana, Mfalme, na Kichwa. Maana ya maneno hayo yote ni kwamba Yesu ni mtawala wa Wakristo wote.
Kazi ya mwili ni nini? Kazi ya mwili ni kutimiza mawazo, mapenzi, na maagizo ya kichwa.
Mwili usioshughulika hauna afya
Jambo moja tunalojua kuhusu miili yetu ni kwamba hatuna raha kama miili yetu haina shughuli za kushughulika nazo. Nani angekuwa na raha kubaki kitandani wiki zima? Mtu akibaki kitandani kwa muda huo tungesema nini kuhusu mtu huyu? Tungesema mtu huyu anaumwa. Mtu mwenye afya hawezi kulala muda wote huo bila kuamka na kufanya shughuli fulani. Ndivyo ilivyo kwa kila Mkristo aliye katika Mwili wa Kristo. Wote wanatakiwa kushughulika wakitii maagizo ya kichwa. Wasipofanya, mwili unakosa afya.
Kila kiungo cha mwili ni muhimu
Tunajua kila sehemu ya mwili lazima ifanye kazi yake ili mwili uwe na afya na maendeleo. Hata sehemu ndogo za mwili ni muhimu na za lazima. Mtu akiumiza kidole chake, mkono wake utashindwa kutimiza kazi yake ipasavyo. Kila kiungo cha mwili kina kazi yake iliyo muhimu. Mungu amepanga mapenzi yake yatimie kupitia mwili wake hapa duniani. Lakini ili mapenzi yake yafanyike ni lazima kila Mkristo atimize wajibu wake.
Mwili unafaulu kazi wakati viungo vinashughulika kwa pamoja
Mwili unafanyaje kazi? Mwili unafanya kazi pale ambapo viungo vyote vya mwili vinafanya kazi kwa pamoja. Kidole hakiwezi kufanya kitu peke yake. Vivyo hivyo na Mkristo hapaswi kuishi peke yake bila Wakristo wengine. Kila Mkristo ameunganishwa na Wakristo wengine katika Mwili wa Kristo ili kwa pamoja watimize mapenzi ya Kristo. Ni katika hali ya ushirikiano Mwili wa Kristo una uwezo mkubwa zaidi. Kwa sababu ni mwili mmoja, Wakristo wanategemeana. Ndiyo sababu Biblia inatoa maagizo kwa Wakristo: kusaidiana, kufundishana, kuonyana, kupendana, kuheshimiana, kuhimizana, kujengana, n.k. Wakifanya hivyo kwa pamoja watafaulu kutimiza mapenzi ya kichwa aliye Yesu Kristo.
Tawi la mahali ni mfano wa Mwili wa Kristo
Kama mshiriki wa Mwili wa Kristo, kila mjumbe ni sehemu ya kundi lile na Yesu anataka kazi zake zitendeke kwa pamoja na katika ummoja. Lakini haiwezekani kila Mkristo ajue na afanye kazi akiwa karibu na kila Mkristo duniani. Kwa sababu hiyo Mungu ameagiza yawepo matawi ya mahali. Wakristo wanapoungana katika matawi ya mahali, wanaweza kutimiza mapenzi ya Mungu kwa njia bora kuliko wanavyoweza kila mtu peke yake. Kusudi la tawi la mahali siyo kukutana na kumwabudu Mungu tu, wala kufundisha Neno la Mungu tu. Kusudi la tawi la mahali ni kutimiza mapenzi yote ya Yesu Kristo. Ni kuabudu, kufundisha Neno la Mungu, na zaidi, likilenga kuhudumia washirika, jamii ya karibu na hata jamii wanaokaa mbali.
Matawi yanaungana kwa baadhi ya kazi
Pia kuna kazi zingine ambazo ni kubwa kiasi ambacho matawi mbalimbali yanahitaji kuungana ili waweze kutimiza mpango wa Mungu kwa ajili ya Mwili wa Kristo.
Mara nyingine Mkristo atatumika peke yake lakini siyo wakati wote
Mfano huu wa Mwili wa Kristo hauna maana kwamba kila wakati Mkristo atakapofanya huduma atakuwa pamoja na Wakristo wenzake. Kwa kuwa Mkristo ni mtumwa wa Kristo masaa yote, ni wazi mara nyingine atahitaji kufanya huduma peke yake. Lakini hawezi kukaa peke yake kila wakati wala kufanya huduma peke yake kila wakati. Mkristo anayekaa peke yake bila ushirikiano wo wote na Wakristo wenzake atapoteza nguvu na kuanguka njiani. Anahitaji msaada wa Wakristo wenzake ili ajengwe na ili huduma zake zipate kufaulu. Ndiyo maana Mungu ameunda Mwili wa Kristo akiwapa karama zilizo mbalimbali na akiwapa uwezo wa kusaidiana na kutegemeana katika kutimiza mapenzi yake.
Maana ya kubatizwa katika Mwili wa Kristo
Tumeona kwamba kila Mkristo ni kiungo au mjumbe wa Mwili wa Kristo. Lakini, Mkristo anapataje kuwa mjumbe? Biblia inasema ni kazi ya Roho Mtakatifu kubatiza Wakristo katika Mwili wa Kristo wakati wanapookolewa.
1 Wakorintho 12:13 – “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru”
Maana ya neno “kubatiza” ni kuchovya au kuweka ndani ya kitu kingine. Roho Mtakatifu anaweka au kubatiza Wakristo ndani ya Mwili wa Kristo wakati wanapookolewa. Ubatizo huo siyo ubatizo wa maji. Wayahudi walipewa agizo la kufanya ubatizo wa maji kama tendo linaloendana na toba wakati walikuwa wakiandaliwa kumpokea masihi wao. Wakati mtu alipobatizwa na maji aliwekwa au kuchovywa katika maji. Lakini wakati mtu anabatizwa na Roho Mtakatifu katika Mwili wa Kristo, mtu huyu anawekwa katika Mwili wa Kristo.
Maana ya kubatizwa katika Mwili wa Kristo: Kazi ya Roho Mtakatifu ya kuweka Mkristo katika Mwili wa Kristo na kumfanya kuwa kiungo au mjumbe wa mwili huo.
Matokeo katika maisha ya Mkristo ya kubatizwa katika Mwili wa Kristo: Mkristo ataelewa ana kazi muhimu ya kutekeleza na atashughulika na kazi hiyo ili mapenzi ya Yesu Kristo, aliye kichwa cha mwili, yapate kutimizwa.
Maswali ya kutafakari: Je, maisha yako yanaoneshaje wewe ni mjumbe wa Mwili wa Kristo anayeshughulika? Una huduma au nafasi gani katika Kanisa?
C. Tunapookolewa Tunaunganishwa Na Kristo
Kabla hatujaokolewa tulikuwa bila Kristo. Tunapookolewa tunaunganishwa na Kristo. Muungano wetu na Kristo ni jambo la ajabu. Inamaanisha kwamba sisi ni ndani ya Kristo (Rum 8:1; 2 Kor 5:17), Kristo ni ndani yetu (Yn 14:20; Gal 2:20), na Mungu Baba na Mwana wanakaa ndani yetu! (Yn 14:23; 1 Yn 4:15, 1 Kor 6:19). Tukifikiria maana ya mambo haya, tutaona kwamba muungano wetu na Kristo ni mkubwa sana.
2 Wakorintho 5:17 – “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”
Wagalatia 2:20 – “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”
Yohana 14:23 – “Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.”
Matokeo ya sisi kuwa ndani ya Kristo ni nini?
Kwa sababu tumo ndani yake, kamwe hatutahukumiwa.
Warumi 8:1 – “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”
Kwa sababu tuko ndani yake kamwe hatutatengwa na Mungu.
Warumi 8:35-39 – “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo?... Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda… Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba… wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Muungano wetu unatupa amani katika maisha yetu kwa sababu hatutakuwa na hofu kwamba tunaweza kupotea.
Kwa sababu tumo ndani ya Kristo, tunabarikiwa na baraka zote za rohoni.
Waefeso 1:3 – “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.”
Baraka za rohoni haziko kama baraka za kimwili. Baraka za kimwili zinadumu kwa muda tu. Baadhi ya baraka za kimwili ni afya nzuri, akili, watoto, mvua n.k. Lakini baraka za rohoni zinadumu milele. Tukiwa ndani ya Kristo, tuna hakika kwamba baraka za rohoni hazitaondolewa. Tunaweza kuzitegemea na kuzifurahia baraka hizo hata milele. Baadhi ya baraka hizo zinatajwa katika Waefeso sura 1:
Kwa sababu tumo ndani ya Kristo, tunapata uwezo wa kuzaa matunda ya kiroho na kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Katika Yohana 15:1-17 Yesu anajifananisha na mzabibu na anatufananisha na matawi. Kama mzabibu unavyoliwezesha tawi kuzaa matunda, vivyo hivyo, Yesu anatuwezesha sisi kuzaa matunda ya kiroho. Yesu alisema kwamba hatuwezi kuzaa matunda ya kiroho isipokuwa tukikaa ndani yake. Matunda ambayo tutayazaa tukiwa ndani ya Yesu ni: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, na upole (Gal 5:22,23).
Maana ya kuungwa na Kristo: Tendo la Mungu la kumweka katika Kristo yule anayemwamini Kristo.
Matokeo ya kuungwa na Kristo katika maisha ya Mkristo: Mkristo atakuwa na amani kwa sababu hawezi kutengwa na Mungu, tena atawezeshwa kuzaa matunda ya kiroho.
Maswali ya kutafakari: Je, una amani na Mungu? Je, matunda gani ya kiroho yanaonekana katika maisha yako?
D. Tunapookolewa, Tunampokea Roho Mtakatifu.
Kila Mkristo anaye Roho Mtakatifu ndani yake
Tunapookolewa, Mungu anatupa Roho Mtakatifu akae ndani yetu. Roho Mtakatifu ni zawadi itokayo kwa Mungu kwa waumini wote. Mungu hawapi baadhi ya Wakristo Roho Mtakatifu, bali kila mmoja anayemwamini Yesu Kristo anapewa Roho Mtakatifu siku hiyo hiyo. Kama mtu hana Roho Mtakatifu, mtu huyu siyo Mkristo (Rum 8:9).
1 Wakorintho 3:16 – “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”
Wagalatia 4:6 – “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.”
Roho Mtakatifu akiingia kwa Mkristo hatoki tena milele
Tuna ahadi ya Yesu kwamba Roho Mtakatifu atakuwa nasi milele.
Yohana 14:16 – “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.”
Baada ya kuja na kukaa ndani yetu, hatatoka tena. Hata kama Mkristo anatenda dhambi, Roho Mtakatifu bado anakaa ndani yake. Mtume Paulo alipowaandikia Wakorintho, aliwauliza kama walijua kwamba miili yao ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yao (1 Kor 6:19). Katikati yao kulikuwa watu waliofanya uovu, hata uzinzi. Swali la mtume Paulo lilionesha kwamba Roho Mtakatifu alikuwa ndani ya wote, hata waliotenda dhambi hizo. Habari hii inaleta amani mioyoni mwetu kwamba Roho Mtakatifu hatatuacha, hata tukifanya dhambi.
Uthibitisho wa kuwa na Roho Mtakatifu
Tunawezaje kuwa na uhakika kwamba tunaye Roho Mtakatifu ndani yetu? Watu wengine wanasema kwamba uthibitisho wa kuwa naye Roho Mtakatifu ni kunena kwa lugha. Lakini Biblia haifundishi kwamba kunena kwa lugha ni uthibitisho wa Roho Mtakatifu kukaa ndani ya Mkristo. Bali Biblia inasema ikiwa mtu hana Roho Mtakatifu ina maana huyu siyo wa Kristo.
Warumi 8:9 – “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”
Hivyo, kila anayemwamini Kristo kweli kweli ni lazima anaye Roho Mtakatifu. Kwa hiyo tuna uhakika tunaye Roho Mtakatifu kama tumemwamini Kristo. Tunao uhakika huo kwa sababu tunaamini ukweli wa Neno la Mungu linaloahidi kwamba wote wanaomwamini Kristo wanaokolewa na kupewa Roho Mtakatifu.
Jambo la pili linalotuhakikishia kwamba tunaye Roho Mtakatifu ni matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Wakati mtu anamwamini Yesu Kristo, Roho Mtakatifu anakuja kukaa ndani ya mtu huyu na anaanza kufanya kazi katika maisha yake. Kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kuzalisha matunda ya Roho ndani ya maisha ya Mkristo. Matunda kama vile upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi (Gal 5:22-23). Matunda ya Roho yataonekana zaidi na zaidi katika maisha ya Mkristo aliye na Roho Mtakatifu ndani yake. Matunda hayo ni uthibitisho wa kuwepo kwa Roho Mtakatifu ndani yake.
Roho Mtakatifu ni muhuri
Waefeso 1:13 – “Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.”
Kila Mkristo anapookolewa anapewa Roho Mtakatifu kuwa muhuri na arabuni (Efe 1:13-14; 2 Kor 1:22). Tuangalie kwanza maana ya “muhuri”. Wakati Rais, mwenyekiti, au katibu anaandika barua, anaitia muhuri wake kama uthibitisho wa kwamba barua hii inatoka kwake. Muhuri unahakikisha kwamba kitu fulani ni cha mtu fulani. Tunapookolewa, tunapewa Roho Mtakatifu kama muhuri wa Mungu kama uthibitisho wa kwamba sisi ni wa Mungu. Mungu anatuahidi kwamba Roho Mtakatifu ni muhuri hata siku ya ukombozi.
Waefeso 4:30- “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.”
Maana yake, Mungu anatuahidi kwamba tutakuwa wa kwake mpaka siku Yesu atakaporudi. Ni muhimu kuelewa Mungu hakusema, “Mpaka siku utakapotenda dhambi.” Yaani, kuwepo kwa Roho Mtakatifu ndani yetu ni uthibitisho wa kwamba hatuwezi kupoteza wokovu wetu na kwamba Mungu atatimiza ahadi zake zote za kutufikisha mbinguni. Mungu hatauondoa muhuri wake, aliye Roho Mtakatifu, kabla Yesu hajarudi kutupeleka mbinguni.
Roho Mtakatifu ni arabuni
Waefeso 1:14 – “Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.”
Roho Mtakatifu pia ni “Arabuni ya urithi wetu.” Arabuni ni nini? Kama mtu anataka kununua kitu fulani na hana hela ya kutosha, analipa kiasi fulani kama arabuni. Arabuni ni kitu ambacho mwenye kununua anatoa kama ahadi kwamba atarudi kuyamalizia malipo. Asiporudi kuyamalizia malipo yale, mwenye kuuza atabaki na hizo pesa alizoziweka. Mungu ametupatia Roho Mtakatifu kama arabuni ya urithi wetu. Maana yake ni kwamba Mungu anatuahidi kwamba tutarithi uzima wa milele. Kwa sasa katika maisha yetu hapa duniani Mungu ametupa Roho Mtakatifu, na kwa kuwa tumempokea Roho, tunaweza kuwa na uhakika kwamba siku moja tutaishi na Mungu mbinguni. Mungu ni mwaminifu. Ataitimiza ahadi yake! Mungu hatamwondoa Roho Mtakatifu. Mungu asipotimiza ahadi yake, kwa kawaida ingekuwa na maana kwamba sisi tungebaki na Roho Mtakatifu kama mali yetu. Jambo hilo haliwezekani kwa sababu Roho Mtakatifu ni Mungu; hatuwezi kummiliki Mungu. Lakini Mungu anapojitoa kama ahadi, anafanya hivyo kwa sababu yeye ana uhakika asilimia mia kwamba atatimiza ahadi yake ya kutufikisha mbinguni. Mungu hayuko katika hatari ya kumpoteza Roho Mtakatifu wake kwa kuwa ana uwezo wa kutimiza ahadi zake.
Kazi za Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu hakai bure ndani yetu. Anatusaidia sana katika maisha yetu ya kikristo. Hapo chini tumetaja baadhi ya kazi anazozifanya kwa ajili yetu wakati anakaa ndani yetu.
Tumshukuru Mungu kwa ajili ya Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu ni zawadi kubwa yenye thamani sana! Tusiache kumshukuru Mungu kwa kutupatia Roho Mtakatifu.
Maana ya kumpokea Roho Mtakatifu: Tendo la Mungu la kumweka Roho Mtakatifu akae ndani ya kila anayemwamini Yesu.
Matokeo ya kumpokea Roho Mtakatifu katika maisha ya Mkristo: Mkristo atakuwa na uhakika kwamba ameokolewa na kwamba hawezi kupotea kamwe. Pia Roho Mtakatifu anasaida kila Mkristo kuishi maisha matakatifu.
Swali la kutafakari: Una uhakika na wokovu wako? Maisha yako yanaoneshaje unaye Roho Mtakatifu ndani yako?
E. Tunapookolewa, Tunahesabiwa Haki.
Warumi 3:24 –“Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.”
Kabla hatujaokolewa, tulikuwa na hatia ya dhambi mbele ya Mungu. Tunapookolewa, Mungu anatuhesabia haki (Rum 3:24, 4:5). Katika kuhesabiwa haki na Mungu kuna sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni kuondolewa hatia ya dhambi. Sehemu ya pili ni kuipokea haki ya Kristo.
Kuhesabiwa haki ni kuifuta hatia tuliyo nayo
Kwanza, Mungu anapomhesabia mtu haki, anasema kwamba yule hana hatia kutokana na dhambi zake tena. Mungu anatangaza mtu yule hataadhibiwa tena kwa sababu Yesu ameichukua adhabu ya dhambi zake zote. Amesamehewa dhambi zake zote kwa sababu deni la dhambi lililipwa kikamilifu kupitia damu ya Yesu Kristo.
Kuhesabiwa haki ni kupewa haki ya Kristo
Ya pili, Mungu anapotuhesabia haki, anatupa haki ya Kristo. Ni kusema, Mungu anaona haki ya Kristo kuwa haki yetu.
2 Wakorintho 5:21 – “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.”
Mungu anatuona tukiwa tumevaa haki ya Yesu siyo haki yetu
Kuhesabiwa haki hakumaanishi kwamba Mungu ametubadilisha kwa ndani ili tuwe wenye haki. Yaani, Mungu hatubadilishi ili matendo yetu yote yawe ya haki. Kuhesabiwa haki kunahusu jinsi Mungu anavyotuona. Mungu anatuona bila hatia ya dhambi, na badala yake anaona haki ya Kristo kuwa haki yetu. Kutokana na matendo yetu sisi siyo wenye haki wala hatuwezi kustahili kuhesabiwa wenye haki. Bali, kwa neema ya Mungu, tunavalishwa haki ya Yesu Kristo na kwa sababu hiyo Mungu anatutangaza kuwa wenye haki.
Kwa neema, wasio na haki (wala uwezo wa kuipata) wanahesabiwa haki na Mungu
Tito 3:6,7 – “…kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.”
Lazima tuelewe kwamba mtu hahesabiwi haki kwa sababu ya haki yake mwenyewe. Sisi hatuna haki hata kidogo mbele ya Mungu, kwa sababu haki zetu ni chafu mbele ya Mungu (Isa 64:6). Mtu hahesabiwi haki kwa sababu amefanya cho chote kuziondoa dhambi zake. Mtu hana namna yo yote ya kuziondoa dhambi na kujisafisha (Rum 10:2-4). Sababu ya kuhesabiwa haki ni neema ya Mungu (Rum 3:24; Tit 3:7). Ni neema ya Mungu iliyomtuma Yesu kufa na kulipa deni la dhambi zetu.
Aliyehesabiwa haki na Mungu hawezi kuwa na hatia tena hata akitenda dhambi
Sisi Wakristo tunapotenda dhambi, Shetani anatushitaki (Ufu 12:10). Kwa sababu ya mashtaka ya Shetani Wakristo wengine wanajisikia kwamba hawastahili kuitwa Wakristo na wanaishi na hofu ya kupotea. Wanajisikia aibu na hatia mbele ya Mungu. Je, tunatakiwa kuishi na hofu, aibu na hatia kwa sababu ya kutenda dhambi? Hapana. Mkristo anayeishi hivyo, hawezi kuishi maisha ya ushindi juu ya dhambi, bali ataishi kama mtu aliyeshindwa dhidi ya Shetani. Hatakuwa na amani na Mungu kama impasavyo. Tena, anakana ukweli wa Warumi 5:1 inayosema kwamba kwa sababu ya kuhesabiwa haki tuna amani na Mungu! Mkristo anayeishi hivyo haamini kwamba Mungu amemsamehe dhambi zake zote, amempa haki ya Kristo na amemtangaza kuwa mwenye haki. Sisi Wakristo hatutakiwi kuishi na hofu kwa sababu ya dhambi tunazozitenda kana kwamba Mungu ataamua kutuhukumu. Hakuna dhambi zinazoweza kumfanya Mungu atuone tena kuwa na hatia ya dhambi. Mungu alipotuhesabia haki, aliziona dhambi zote tulizozitenda na dhambi zote tutakazozitenda na alitusamehe zote!
Kutoweza kupata hatia tena hairuhusu Wakristo kutenda dhambi
Kama hatutakiwi kuwa na hofu, aibu, wala hatia tunapotenda dhambi, tunatakiwa kufanya nini? Tunaweza kutojali dhambi au kufurahia dhambi? Hapana! Tu watumwa wa Mungu na kama watumwa wake tunapotenda dhambi, tunatakiwa kujisikia kama Mungu anavyojisikia. Tunapaswa kuchukia dhambi na kuhuzunika wakati tunapotenda dhambi. Mungu ni Mtakatifu na anataka sisi tuwe watakatifu katika matendo yetu. Tutawezaje kuishi katika dhambi wakati Yesu aligharimu maisha yake kwa ajili ya kutukomboa na dhambi? Kutotenda dhambi kwetu ni njia ya kuonesha shukrani yetu kwa Mungu aliyetuokoa. Kama Wakristo, tunapotenda dhambi, tunapaswa kuungama dhambi yetu. Hatufanyi hivyo kwa ajili ya kukwepa hukumu ya Mungu wala kwa ajili ya kuokoka. Mungu alishasamehe dhambi hizo na kutuahidi hatutahukumiwa naye tena na zaidi ameahidi hatuwezi kupoteza wokovu wetu. Bali kuungama dhambi zetu kama Wakristo ni kwa ajili ya kutengeneza uhusiano wetu na Mungu kama mwana na baba yake. Hatujapoteza uwana wetu lakini kuungama dhambi zetu kunatusaidia kuboresha uhusiano ule unaoendelea na Mungu. Pia kuungama dhambi zetu kama Wakristo kunapunguza uwezekano wa Mungu kutuadhibu kama wana (Ebr 12:5-11). Adhabu hiyo si ya hasira bali ni ya upendo (Ebr 12:6). Adhabu hiyo siyo hukumu ya kuangamiza bali ni yenye kusudi la kuwa faida yetu, “ili tuushiriki utakatifu wake” (Ebr 12:10).
Maana ya kuhesabiwa haki: Tendo la Mungu la kumtangaza kuwa mwenye haki yule anayemwamini Yesu Kristo kwa sababu Mungu ameiondoa hatia ya dhambi yake na kumpa haki ya Kristo.
Matokeo ya kuhesabiwa haki katika maisha ya Mkristo: Mkristo ataishi na amani bila hofu ya kupotea, wala hatia au aibu mbele ya Mungu.
Swali la kutafakari: Unapotenda dhambi, je, unaogopa utapoteza wokovu wako?
F. Tunapookolewa, Tunatakaswa.
Maana ya utakaso
Neno “utakaso” au “kutakasa” linamaanisha “kufanya takatifu.” Tunaposema kwamba tumetakaswa, tunasema kwamba tumefanywa watakatifu na ndiyo maana Biblia huita Wakristo watakatifu (2 Kor 1:1; Efe 1:1; Flp 4:21,22).
Utakaso kamili siku ya kuokoka
Biblia inafundisha kwamba kuna aina mbili za utakaso wa Mkristo. Aina moja inahusika na wokovu. Aina hii ni utakaso kamili unaotendeka wakati tunapookolewa.
1 Wakorintho 6:11 – “Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.”
Utakaso huo unakamilika mara moja, yaani ni tendo lilioisha.
Mungu anawahesabu Wakristo kuwa Watakatifu
Utakaso huo unafananishwa na kuhesabiwa haki na ni tangazo la Mungu kwamba huyu aliyemwamini Yesu anaonekana safi machoni pa Mungu, ndiyo sababu Mungu anaweza kuwaita Wakristo “watakatifu”. Ingawa siyo hali halisi ya Wakristo katika maisha yao, ni tamko la Mungu kama hakimu katika mahakama yake.
Utakaso huo siyo mabadiliko ya ndani ya mioyo yetu kutufanya tuwe safi bali ni mabadiliko katika jinsi Mungu anavyotuona. Mungu hatuoni kuwa wachafu tena. Anatuona kuwa watakatifu. Si kwamba hatufanyi dhambi tena, lakini Mungu anatuona kama vile hatuna dhambi.
Mungu anaweza kutuhesabu Watakatifu kwa kuwa alikufa kwa ajili ya dhambi zetu zote
Waebrania 10:10 – “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.”
Je, Mungu anawezaje kutuona kuwa watakatifu ingawa tunaendelea kutenda dhambi? Tutaangalia tena mfano tuliotumia tulipoichunguza kazi ya Yesu msalabani. Tuliona kwamba Yesu alizichukua akiadhibiwa kwa ajili ya dhambi zetu na kwa njia hiyo akaondoa dhambi na hatia yetu akitupa msamaha wa dhambi zetu. Kwa sababu hiyo tumesafishwa dhambi zetu zote; dhambi tulizozitenda wakati uliopita, na dhambi tutakazozitenda wakati ujao.

- Tumechaguliwa naye (1:4)
- Tumefanywa kuwa watakatifu (1:4)
- Tumefanywa kutokuwa na hatia (1:4)
- Tumefanywa kuwa wana (1:5)
- Tumepewa ukombozi (1:7)
- Tumepewa msamaha wa dhambi (1:7)
- Tumefanywa warithi (1:11)
- Tumefanywa sifa ya utukufu wa Kristo (1:12)
- Tumeokolewa (1:13)
- Tumepewa Roho Mtakatifu kama arabuni ya urithi wetu (1:14)
- n.k.

- Anatujaza (Efe 5:18)
- Anatuongoza (Rum 8:14)
- Anatupa uhakika wa wokovu wetu (Rum 8:16)
- Anatusaidia kuomba (Rum 8:26)
- Anatuwezesha kuzaa matunda ya kiroho (Gal 5:22,23)
- Anatuwezesha kutozitimiza tamaa za mwili (Rum 8:13; Gal 5:16).

Mchoro#13 - Mchoro huu unaonesha dhambi tulizozitenda, tunazozitenda, na tutakazozitenda zimelipiwa na sasa machoni pa Mungu sisi ni watakatifu tusio na hatia ya dhambi.
Tumesema Mungu kama hakimu anatamka katika mahakama yake kwamba wote wanaomwamini Yesu ni wenye haki, ni watakatifu, na ni waliotakaswa. Tamko hilo linawezeshwa na kazi ya Yesu kuwalipia deni la dhambi zao na kuwashirikisha katika haki, utakatifu, na usafi wake. Kumbe baada ya kuokoka Mungu anapotuangalia anaona haki, utakatifu, na usafi wa Yesu kana kwamba ni haki, utakatifu, na usafi wetu.
Hali hii inawezekana kwa sababu sisi Wakristo tumeunganishwa na Kristo. Tumo ndani ya Kristo na Kristo yumo ndani yetu. Mungu anapotuona, hatuoni peke yetu, bali anatuona pamoja na Kristo. Ndiyo maana anauona utakatifu wa Kristo kuwa wa kwetu.
1 Wakorintho 1:30 – “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi.”
Wagalatia 3:27 – “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo”
Mfano wa Wakorintho - Watakatifu wanaotenda dhambi
Biblia inatumia neno “Watakatifu” kueleza wale ambao wametakaswa na Mungu. Neno hilo linatumiwa kwa Wakristo wote na si kwa wale tu wanaofaulu zaidi katika kutotenda dhambi (2 Kor 1:1, Efe 1:1, Flp 4:21-22; Kol 1:22, Ebr 10:10). Mungu anawaita Wakristo watakatifu ingawa bado wanatenda dhambi kwa sababu wamesafishwa dhambi zao kwa damu ya Kristo na kwa sababu wamo ndani ya Kristo. Ndiyo sababu mtume Paulo aliweza kuwaita Wakorintho “wale waliotakaswa katika Kristo Yesu” (1 Kor 1:2). Je, Wakorintho walikuwa watu ambao waliishi maisha makamilifu bila dhambi? Hapana. Wengine kati yao walikuwa na tabia mbaya sana. Mtume Paulo aliwakemea mara nyingi kwa sababu walikuwa wanaishi maisha maovu. Kwa sababu ya uovu wao mtume Paulo aliwaita “watu wenye tabia ya mwilini” (1 Kor 3:1-3)! Kweli hawakuishi maisha makamilifu, lakini bado walikuwa watakatifu kwa sababu walisafishwa dhambi zao na walikuwa ndani ya Kristo. Ndiyo sababu Mungu aliwaona kuwa watakatifu.
Mfano wako - Mtakatifu anayetenda dhambi
Hatupaswi kuangalia Wakorintho kujua kwamba Wakristo (watu ambao wametakaswa) hawaishi maisha makamilifu kila wakati. Kila mmoja tunaweza kujiangalia wenyewe na kujua “kutakaswa” siyo kuishi bila dhambi. Mtakatifu ni Mkristo aliye safi machoni pa Mungu kwa sababu ya Kristo, si kwa sababu ya matendo yake mwenyewe kama Mkristo.
Mtakatifu anaweza kushirikiana na Mungu
Kumbuka kwamba mwanadamu anapaswa kuwa mtakatifu ili aweze kushirikiana na Mungu. Tunapookolewa, tunatakaswa (tunafanywa watakatifu) machoni pa Mungu. Ndiyo sababu Mungu anaweza kushirikiana na wote wanaomwamini Yesu na kuwa na uhusiano nao.
Utakaso wa siku hadi siku katika maisha ya Mkristo
2 Wakorintho 7:1- “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”
Aina ya pili ya utakaso ni utakaso unaoendelea muda wote katika maisha ya Mkristo. Unaeleza hali ya Mkristo anavyobadilika polepole katika maisha yake ili afanane na Yesu na aishi kwa namna inayompendeza Mungu. Mistari mingi sana inaeleza wajibu wa Mkristo kujitakasa kwa kuachana na dhambi (2 Kor 7:1, 1 Pet 2:11), kwa kujitoa kwa Mungu na kufanya nia yao upya (Rum 12:1-2), kwa kukua kiroho (1 Pet 2:2), kwa kufuata haki, utauwa, imani, upendo saburi n.k. (1 Tim 6:11-12), kwa kuishi kwa ajili ya Mungu (Gal 2:20), kwa kumfuata Mungu (Efe 5:1-2) kwa kumwiga Yesu (2 Kor 3:17-18; Rum 8:9; Efe 5:2; Flp 2:5-8) na mambo mengine mengi tusiyoweza kuyataja hapa.
Mungu anatusaidia kufaulu katika shughuli ya utakaso huo. Tulishaona jinsi tulivyopewa Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu ili atusaidie kuishi jinsi Mungu anavyotaka, lakini hata Yesu anatusaidia na ataendelea kutusaidia mpaka siku ya mwisho.
Wafilipi 1:6 – “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu”
Utakaso huo hautakamilika mpaka Mungu atakapowapa Wakristo miili ya utukufu siku ambayo Kristo atanyakua Kanisa lake. Siku ile tutafanana na Kristo kweli kweli na tutaitwa watakatifu kwa sababu kweli kweli tutakuwa watakatifu. Kwa sasa, sisi Wakristo hatujakamilika, lakini kwa uwezo wa Mungu tunabadilika siku hadi siku tukifuata maagizo ya Mungu.
Maana ya kutakaswa: Tendo la Mungu kumfanya mtakatifu, machoni pake, yule anayemwamini Kristo kwa sababu ya damu ya Kristo na muungano wa Mkristo na Kristo.
Matokeo ya kutakaswa katika maisha ya Mkristo: Mkristo anaweza kushirikiana na Mungu mtakatifu.
Swali la kutafakari: Maisha yako yanaoneshaje jinsi unavyoshirikiana na Mungu?
G. Tunapookolewa, Tunafanywa Wana.
Tunazaliwa tukiwa wana wa Shetani
Tunapookolewa Mungu anatufanya kuwa wana wake. Watu wengine wanawaza kwamba sisi sote ni wana wa Mungu tangu kuzaliwa kwetu. Lakini Biblia inafundisha kwamba tulizaliwa tukiwa wana wa Shetani (Yn 8:44) tena tukiwa na asili ya dhambi (Rum 5:12). Ni wakati tunapookolewa Mungu anatuingiza katika jamaa yake na kutufanya kuwa wana.
Kuwa mtoto wa Mungu ni kuwa mrithi wake
Wagalatia 4:7 – “Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”
Kwa sababu tumekuwa wana wa Mungu, Biblia inatufundisha kwamba sisi ni warithi wa Mungu. Tunarithi nini? Urithi wetu ni wokovu, yaani uzima wa milele (Ebr 1:14; Tit 3:7).
Kama warithi wa wokovu tutaishi na Mungu milele mbinguni. Urithi wa kidunia, kama mali au pesa, unaweza kuharibika na kupotea, lakini Mungu anatunza urithi wetu na hauwezi kuharibika (1 Pet 1:3,4). Utadumu milele (Ebr 9:15).
Kuwa mtoto wa Mungu ina maana tunahusiana na Mungu bila hofu
Warumi 8:14,15 – “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.”
Kwa sababu tumekuwa wana wa Mungu, tuna uhusiano maalumu na Mungu. Hatutakiwi kumwogopa Mungu tena. Uhusiano wetu ni zaidi ya kuwa na ushirikiano na Muumba wetu, ni zaidi ya kuwa na ushirikiano na Mtawala mkuu, na ni zaidi ya kuwa na ushikiriano na hakimu mkuu. Uhusiano wetu na Mungu ni wa karibu sana kama uhusiano kati ya mtoto na baba yake. Ndiyo sababu tunaweza kumwita Mungu “baba”. Tunaweza kustarehe katika upendo mkamilifu wa Mungu unaozidi hata upendo wa wazazi wetu hapa duniani.
Maana ya kufanywa wana: Tendo la Mungu la kumfanya kuwa mwana mrithi yule anayemwamini Kristo.
Matokeo ya kufanywa mwana katika maisha ya Mkristo: Mkristo atastarehe katika upendo wa Mungu, Baba yake, na kuufurahia uhusiano wa karibu na Mungu.
Swali la kutafakari: Je, unafurahia uhusiano wako na Mungu kama mtoto anayependwa naye?
H. Tunapookolewa Tunasamehewa Dhambi Zetu
Wakati tunapookolewa Mungu anatusamehe dhambi zetu zote (Mdo 10:43; 13,38; 26:18; Efe 1:7; Kol 1:14; 2:13). Hatusamehewi dhambi zile tu tulizotenda kabla hatujazaliwa, bali tunasamehewa hata dhambi zile ambazo hatujazitenda bado. Katika kusamehe dhambi zetu Mungu anatangaza kwamba malipo yamelipwa na yamekubaliwa asilimia mia. Hatuwezi kuhukumiwa tena kwa ajili ya dhambi zetu kwa kuwa Mungu alishazisamehe zote.
Mungu anawezaje kusamehe dhambi zetu zote wakati tunapookolewa? Anaweza kuzisaheme zote kwa kuwa alishazihukumu katika Yesu msalabani.
Maana ya kusamehewa dhambi zetu zote: Tendo la Mungu kusamehe dhambi zote za Wakristo kwa sababu dhambi hizo ziliadhibiwa katika Yesu Kristo msalabani.
Matokeo ya kusamehewa dhambi zote katika maisha ya Mkristo: Wakristo wanaweza kuishi bila kuhofu kwa maana hawatahukumiwa kwa kuwa dhambi zao zote zimeshasamehewa (zilizotendeka, zinazotendeka, na zitakazotendeka).
Maswali ya kutafakari: Je, unaamini ahadi ya Mungu kwamba alishasamehe dhambi zako zote? Je, unamshukuru Mungu kwa zawadi hiyo ya ajabu?