GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU

- 14 -

Wokovu Unaleta Mabadiliko Gani Katika Uhusiano Wetu na Shetani na Dhambi?

Kila mtu anazaliwa akiwa chini ya mamlaka ya Shetani na dhambi

Tunapookolewa, tunakombolewa kutoka katika mamlaka ya Shetani na dhambi. Kwa sababu Adamu aliamua kumfuata Shetani na kumwasi Mungu, alikuwa mwenye dhambi.

Warumi 5:12 - “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.”

Adamu alipokea asili ya dhambi inayoitwa “utu wa kale” au “mwili” katika Biblia. Dhambi ilianza kumtawala na alikuwa mtumwa wa dhambi. Pia, Adamu alipomfuata Shetani, alijiweka chini ya mamlaka yake, hivyo Shetani alikuwa mtawala wake. Kwa sababu ya dhambi ya Adamu, wazao wake wote wanazaliwa wakiwa na asili ya dhambi, wakiwa chini ya utawala wa Shetani, na watumwa wa dhambi.

Kutawaliwa na Shetani na dhambi ni kuwatumikia

Inamaanisha nini kuwa chini ya utawala wa Shetani na kuwa mtumwa wa dhambi? Inamaanisha kwamba sisi tunaishi maisha ya kuyafuata mapenzi ya Shetani na dhambi na pia tunatii Shetani na dhambi. Tunafanya dhambi na kuifurahia. Kwa nini? Kwa sababu ndivyo watawala wetu wanavyotaka kwetu.

Aliyeokoka hatawaliwi na Shetani tena

Tunapookolewa, Mungu anatukomboa kutoka katika mamlaka ya Shetani na utumwa wa dhambi.

Warumi 6:6-7 – “utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.”

Hii inamaanisha nini? Kwanza, Shetani siyo mtawala wetu tena. Kristo alimshinda Shetani na pepo wote msalabani (Kol 2:15; Ebr 2:14-15). Hivyo, kama Wakristo, hatupaswi kuwatii, kuwatumikia, wala kuwaogopa Shetani na pepo tena. Tuko huru na mamlaka yao.

Mfano huu utatusaidia kuelewa ni mabadiliko gani yanayotokea kwenye uhusiano wa Mkristo na Shetani wakati Mkristo anapookolewa. Nimetunga mfano huu mwenyewe kuhusu mtoza ushuru anayeitwa Anatory.

Anatory alikuwa mtoza ushuru vijijini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mwaka 1990 na kuendelea. Alikuwa mtu mwovu na mara nyingi alidai kodi kuliko watu walivyopaswa kulipa kulingana na sheria. Hata wale ambao hawakutakiwa kulipa kodi, aliwatoza kwa nguvu. Watu hawakumpenda kabisa lakini hawakuweza kumfanya cho chote kwa kuwa alikuwa mtumishi wa serikali aliyekubaliwa na wakubwa wake.

Katika mwaka 1996 vita ilianza katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye kusudi la kumfukuza rais wao. Wakati wapinzani walipokaribia mji mkuu, Anatory alijua siku zake za kufanya kazi serikalini zilikuwa zinaisha. Tarehe 17 ya mwezi Mei wapinzani walishinda jeshi la serikali.

Wakati Anatory alipoamka tarehe 17 ya mwezi Mei, alijua amepoteza kazi yake. Lakini kwa kuwa habari zilifika vijijini polepole alifanya safari ya mwisho kukusanya kodi kabla habari zile hazijafika.

Alifika katika kijiji cha kwanza asubuhi na mapema. Mtu wa kwanza aliyekutana naye akamdai kuku. Kwa sababu hakujua Anatory hakuwa na mamlaka, mtu huyu alimpa kuku. Anatory alipanga kupitia vijiji vingi siku ile akidai pesa na chakula kama malipo ya kodi za watu ili abaki nazo mwenyewe.

Alipofika katika kijiji cha pili watu walikuwa wameshasikia habari za kuanguka kwa serikali. Lakini Anatory aliamua kuwadai ingawa alijua wanafahamu habari hizo. Pamoja na kwamba watu walijua Anatory hakuwa na mamlaka juu yao tena mmoja alikuwa amezoea kumwogopa na hivyo kutokana na hofu yake alikubali kumlipa.

Lakini wengine waliitika tofauti. Wakati Anatory alipowaendea waliwaita majirani wao waje kusaidia kumpiga Anatory na kumfukuza kijijini. Anatory alikuwa amepoteza mamlaka yake na hawakuweza kumkubali tena. Anatory alikimbia akijua wanaweza hata kumwua.

Katika hadithi hii Anatory ni mfano wa Shetani na wanakijiji ni Wakristo. Wakristo wote wamewekwa huru na Shetani, hawako chini ya mamlaka yake tena. Lakini Wakristo wengine wanamwitikia Shetani kama wanakijiji wa kijiji cha kwanza. Hawajui kwamba wamewekwa huru na Shetani na hivyo wanaendelea kumruhusu Shetani kuwatawala na kuwashawishi kutenda dhambi, yaani wenyewe wanakubali kumtii. Wakristo wengine ni kama yule mmoja katika kijiji cha pili. Wanajua kwamba Shetani hana mamlaka juu yao tena lakini kwa sababu mbalimbali wanaamua kumtii Shetani badala ya kumtii Mungu, yaani, wanampa Shetani utawala wakati hanao. Lakini Mungu anataka Wakristo wote kuwa kama wale wengine katika kijiji cha pili. Wajue Shetani hana mamlaka juu yao na hivyo wamfukuze katika maisha yao kwa kukataa kumtii. Yakobo 4:7-8 inasema,
“Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu.”
Pili, tunapookolewa sisi si watumwa wa dhambi tena. Yesu alipokufa, utu wa kale ulisulubishwa pamoja naye (Rum 6:6-7; Gal 5:24). Kusulubiwa kwa utu wa kale kuliuvunja utawala wa dhambi juu yetu. Tunakuwa huru na dhambi. Hivyo hatupaswi tena kufanya dhambi kwa kuwa dhambi au utu wa kale hauwezi kutulazimisha kufanya dhambi.

Aliyekombolewa yuko huru

Kukombolewa kutoka katika mamlaka ya Shetani na dhambi ni kuwekwa HURU na mamlaka ya Shetani na dhambi katika maisha yetu. Inawezekana sasa kuishi tukiwa huru bila kutenda dhambi!

Warumi 6:22 – “Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.”

Maana ya kukombolewa kutoka katika mamlaka ya Shetani na dhambi: Tendo la Mungu la kumfanya yule anayemwamini Kristo kuwa huru na mamlaka ya Shetani na dhambi katika maisha yake.

Matokeo ya kukombolewa kutoka katika mamlaka ya Shetani na dhambi katika maisha ya Mkristo: Mkristo ataweza kuishi maisha huru bila kulazimishwa kutenda dhambi kwa sababu hatawaliwi na Shetani wala dhambi tena.

Swali la Kutafakari: Maisha yako yanaoneshaje kwamba uko huru na utawala wa Shetani na dhambi?


RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 15
Proudly powered by Weebly