WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU
- 12 -
Toba Inahusikaje Katika Wokovu?
Kutubu hakuleti wokovu
Mtu akipenda kuokolewa, anatakiwa kufanya nini? Watu wengi watajibu kwamba anatakiwa kutubu. Lakini Biblia inafundisha kwamba kuna sharti moja tu ili aupokee wokovu. Sharti hilo ni kuiweka imani katika Bwana Yesu: “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka” (Mdo 16:31).
Toba siyo njia ya kuokoka. Kama tulivyokwishajifunza, imani ni njia peke ya kuokoka. Lakini imani ya kweli, inayoleta wokovu, inatakiwa ijengwe juu ya msingi wa toba. Mtu akikosa kutubu, anaweza kuamini bure. Basi, tuchunguze kwanza maana ya toba au kutubu.
Wengi wanachanganyikiwa siku hizi kuhusu maana ya “kutubu” kwa jinsi inavyohusika katika wokovu. Wakristo wengine wanasema kwamba kutubu ni kuacha dhambi. Wengine wanasema kutubu ni majuto.
Tutaanza kwa kuyachunguza mawazo haya kuhusu toba na kuona kwa nini mawazo haya siyo sahihi. Baada ya hayo, tutajifunza yale Biblia inayofundisha kuhusu toba.
Kutubu si kuacha dhambi
Wengine wanasema kutubu ni kuacha kutenda dhambi. Wanadai kabla mtu hajaja kwa Kristo na kumwamini ni lazima aachane na dhambi ndani ya maisha yake kwanza. Yaani, wanaamini ni lazima mtu abadilike kabla hajaokoka. Lakini tutaona ufafanuzi huo siyo sahihi kwa sababu wanadamu, peke yao, hawawezi kuacha kutenda dhambi asilimia mia katika maisha yao.
Ingekuwa kweli kwamba maana ya kutubu ni kuacha kutenda dhambi, matokeo yake ni kwamba hakuna ambaye angeweza kuokoka. Kwa nini? Kwa sababu Biblia inasema wote wasioamini wamekufa kiroho na wako chini ya utawala wa Shetani. Ni lazima wasiomwamini Yesu wamtii mtawala wao, yaani, ni lazima watende dhambi. Hivyo, wasioamini hawawezi kuacha kutenda dhambi kwa kuwa wanatawaliwa na Shetani na hali yao ya kuwa watumwa wa dhambi. Hakuna kati yetu, hata Mkristo mmoja, ambaye ameacha kutenda dhambi asilimia mia. Ikiwa sisi Wakristo, tulio na Roho Mtakatifu ndani yetu, hatuwezi kuacha kutenda dhambi, je, atawezaje asiyeamini ambaye ni mtumwa wa Shetani? Jibu ni kwamba hawezi kuacha kutenda dhambi. Hivyo, maana ya kutubu haiwezi kuwa kuacha kutenda dhambi. Mungu hawezi kumdai mwanadamu kitu asichokiweza.
Kutubu si majuto wala huzuni
Mara nyingi huzuni au majuto yanasindikiza toba. Lakini huzuni au majuto siyo toba yenyewe. 2 Wakorintho 7:10 inasema: “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.” Hapa Biblia inataja aina mbili za huzuni. Aina moja ya huzuni ni “huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu.” Huzuni hii inatangulia na kuleta toba, lakini siyo toba yenyewe. Huzuni ya pili inaitwa “huzuni ya dunia.” Huzuni hii siyo toba wala haileti toba. Inaleta mauti. Maana yake, huzuni hii ni huzuni ya mtu anayehuzunika bila kutubu.
Katika Mathayo 19:16-26, kijana tajiri alimwuliza Yesu afanye kitu gani chema ili apate uzima wa milele. Alikuwa anayategemea matendo mema ili aokolewe. Yesu alitumia sheria kumwonesha matakwa makamilifu ya Mungu. Baada ya kusikia yale aliyotakiwa kuyafanya, hakupenda kuyatimiza. Kijana huyu alienda zake kwa huzuni. Huzuni ya kijana tajiri ilileta toba? Hapana. Alikuwa na huzuni ya aina gani? Huzuni ya kidunia. Tumeona kwamba huzuni au majuto siyo toba. Huzuni inaweza kuleta toba au kuisindikiza toba, lakini pia mara nyingine huzuni haifuatani na toba.
Kutubu ni kuyabadilisha mawazo
Tumeona kwamba kutubu siyo kuacha dhambi wala kuwa na hisia za huzuni. Sasa, tuone yale Biblia inayofundisha kuhusu toba. Maana ya neno “kutubu” katika Agano Jipya ni “kubadili mawazo”. Toba ni mabadiliko ya mawazo kuhusu tendo, neno, au uamuzi fulani. Kwa mfano, mtu fulani anaweza kutenda tendo ambalo halioni kuwa baya, kusema neno ambalo halioni kuwa baya, kuamua jambo ambalo halioni kuwa baya, au kuishi maisha ambayo hayaoni kuwa mabaya. Lakini, baadaye anaweza kufika mahali pa kugundua kwamba tendo, au neno, au uamuzi, au maisha yake, kweli yalikuwa mabaya. Mabadiliko yake katika mawazo haya ni toba. Kwa mfano mwingine, mtu anaweza kuamua kufanya kitu fulani lakini baadaye anabadili uamuzi wake. Tunasema kwamba mtu yule ametubu. Mabadiliko ya mawazo yake ni toba. Tazama kwamba toba ni mabadiliko ya ndani; ni mabadiliko ya mawazo au mtazamo na siyo mabadiliko ya matendo.
Mifano ya toba katika Biblia
Tutaangalia sasa mifano ya matumizi ya neno “toba” au “kutubu” katika Biblia. Mifano hii itatusaidia kufahamu kwamba kutubu ni kuyabadili mawazo.
Mfano wa toba katika maisha ya Sulemani
Tunapata mfano mzuri wa maana ya toba katika 1 Wafalme 8:46-49. Mfalme Sulemani alikuwa amemaliza kujenga hekalu. Aliwaita Waisraeli wote kusherehekea kuliweka wakfu hekalu. Mfalme Sulemani alisali na akamwomba Mungu hivi:
“Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu; basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliwachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu; watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao.”
Katika sala yake, Mfalme Sulemani anataja uwezekano wa Waisraeli kuacha kumfuata Mungu na kuziabudu sanamu. Ikiwa watafanya hivyo na ikiwa Mungu atawaadhibu, alisema kwamba inawezekana “watajirudia nafsi zao”. Maana ya “kujirudia nafsi zao” ni nini? Ni kubadilisha mawazo yao kuhusu uovu wao. Ndiyo kutubu. Kutubu kwao kutahitajika wakimkosea Mungu kwa kuabudu miungu ya uongo bila kujali. Wanapofika mahali pa kugundua kwamba walikuwa wamefanya vibaya, ndipo wangetubu na kusema, “Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu.” Toba yao inatoka ndani yao. Ikiwa ni toba ya kweli, Mfalme Sulemani alisema itaoneshwa kwa jinsi watakavyomrejea Mungu. Kurejea kwa Mungu siyo toba, lakini ni matunda ya toba yao ya kweli.
Mfano wa toba katika mifano ya Yesu
Bwana Yesu alitoa mfano wa kijana aliyetubu (Mt 21:28-32). Kijana huyo alikuwa amesema kwamba hatatumika shambani mwa baba yake, lakini baadaye alitubu, na akaenda shambani. Maana yake, aliyabadili mawazo yake na alikubali kufanya kazi shambani. Hapa tunaona kwamba kutubu kunamaanisha kuyabadili mawazo. Je, kijana aliachana na dhambi? Hapana. Je, alijutia dhambi zake? Hapana. Kijana alibadili mawazo yake kuhusu jibu ambalo alikuwa amempa baba yake na baada ya kuyabadili mawazo akafanya kazi.
Mfano wa toba katika Luka
Mfano mwingine wa toba ni katika Luka 17:3-4:
“Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.”
Hapa anayetubu anatubu kwa ajili ya nini? Anatubu kuhusu kosa alilomtendea mwingine. Anayabadili mawazo na kuona kwamba tendo alilomtendea mwenzake lilikuwa baya; kwa hiyo anautafuta msamaha.
Jumla ya fundisho la mifano hii
Mifano hii inathibitisha kwamba maana ya kutubu ni kuyabadili mawazo. Mifano hii inaonesha pia kwamba toba ni mabadiliko yanayofanyika ndani ya mtu, siyo mabadiliko ya nje. Ni mabadiliko ya mawazo, siyo mabadiliko ya matendo. Mabadiliko ya matendo ni tokeo la toba, lakini siyo toba yenyewe.
Toba iliyo msingi wa imani
Katika mifano ya hapo juu, watu wanatubu kwa ajili ya mambo mbalimbali (kuabudu sanamu, kutofanya kazi shambani, kumkosea mwingine). Katika mifano hii, toba yao siyo toba inayohusiana na wokovu. Sasa tunataka kuangalia toba inayohusiana na wokovu. Tunajua kwamba toba inatangulia imani inayoleta wokovu, na tunajua kwamba toba ni mabadiliko ya mawazo. Basi, toba hiyo inayotangulia imani iletayo wokovu ni mabadiliko ya mawazo gani? Ni kubadili mawazo kuhusu nini?
Toba ni kuyabadili mawazo kuhusu upekee wa Mungu
Watu wanaweza kuwa na mawazo mengi ya uongo kuhusu Mungu. Lakini anayependa kuokolewa anatakiwa kuyabadili mawazo yake kuhusu Mungu ili yafuatane na ukweli wa Biblia. Kwanza mtu anatakiwa kukubali kwamba Mungu ni mmoja na hakuna mwingine. Kama mtu anaamini Mungu wa Biblia ni mmojwapo miongoni mwa miungu mingi, kweli hajui jambo hilo la msingi kuhusu Mungu.
Waisraeli walizungukwa na watu walioiabudu miungu ya uongo. Kabla hawajaingia nchi ya ahadi, Mungu alisisitiza kwamba yeye pekee ni Mungu katika Kumbukumbu la Torati 6:4. Kifungu hiki ni msingi wa imani ya Kiyahudi. Kinasema, “Sikiliza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja.” Wengine hawaoni umuhimu wa kuwashuhudia watu kwamba Mungu ni mmoja. Tukichunguza huduma na mahubiri ya Bwana Yesu, tunaona kwamba yeye hakuwafundisha Wayahudi kwamba Mungu ni mmoja. Kwa nini? Kwa sababu Wayahudi tayari waliamini kwamba Mungu ni mmoja. Mtume Paulo alizoea kuwahubiria watu waliokusanyika kwenye masinagogi. Alipowahubiria Injili, je, alianza na mafundisho kwamba Mungu ni mmoja? Hapana. Kwa nini? Kwa sababu wale waliohudhuria katika masinagogi tayari walijua kwamba Mungu ni mmoja. Lakini, wakati mtume Paulo alipowashuhudia wapagani wa Athene, watu ambao waliabudu miungu mbalimbali bila kumjua Mungu wa kweli, alianza kwa kuwashuhudia nini (Mdo 17:22-34)? Je, alianza kwa kushuhudia kwamba walikuwa wenye dhambi na kwamba Kristo alikufa kwa ajili yao? Hapana. Hakulitaja jina la Yesu. Alianza kwa kuwafundisha kuhusu Mungu wa kweli.
Hii ina maana kwetu sisi kwa sababu watu wengine hapa Tanzania wanaabudu miungu ya uongo. Sisi wainjilisti tunatakiwa kugundua kwanza kama yule tunayemshuhudia anaamini kwamba Mungu ni wa pekee. Mtu akiunganisha imani katika Yesu na imani yake katika miungu mingine, je, Mungu atamfurahia na kumkubali? Hapana, mtu yule atakuwa anaamini bure. Hivyo lazima mtu anayekuja kwa Kristo atubu na kubadili mawazo yake kuhusu ummoja na upekee wa Mungu wa kweli.
Toba ni kuyabadili mawazo kuhusu utakatifu wa Mungu
Jambo la pili ambalo mtu anapaswa kuyabadili mawazo yake ni utakatifu wa Mungu. Watu wengi hawaufahamu ukweli wa kwamba Mungu ni mtakatifu. Wanafikiri kwamba Mungu atawakubali ingawa wametenda dhambi. Wanatakiwa kuyabadili mawazo yao na kukubali kwamba Mungu mtakatifu hawezi kushirikiana na mwenye dhambi. Inabidi mtu aelewe ni lazima awe mtakatifu ili aweze kushirikiana na Mungu. Hata kama anajitahidi kumpendeza Mungu, jitihada zake ni bure kwa sababu yeye bado ni mwenye dhambi na mchafu mbele za Mungu. Mungu hatamkubali hata kidogo asipokuwa mtakatifu. Katika kuyabadili mawazo yake kuhusu utakatifu wa Mungu, badala ya kujitegemea kujifanya sawa mbele ya Mungu, mtu anatakiwa amtegemee Mungu kumfanya mtakatifu.
Toba ni kuyabadili mawazo kuhusu haki ya Mungu
Jambo la tatu ambalo mtu anatakiwa kuyabadili mawazo yake ni haki ya Mungu. Wengine wanafikiri kwamba Mungu ataachilia dhambi zao wakizichanganya na matendo mema. Wanapaswa kuyabadili mawazo haya na kukubali kwamba Mungu ni mwenye haki, yaani Mungu anadai dhambi zote ziadhibiwe. Adhabu ya dhambi ni mauti; yaani kutengwa na Mungu milele motoni. Kwa sababu Mungu anadai kila dhambi iadhibiwe, mtu hawezi kujitetea mbele ya Mungu. Mtu asidhani kwamba ataweza kujifanya akubaliwe na Mungu kwa sababu ya matendo yake mema. Yule anayeyategemea matendo yake mema kumwokoa, anahitaji kuulizwa namna gani matendo yake yataifuta adhabu ya dhambi zake. Mwisho anapaswa kutubu mawazo haya na kuyabadilisha ili mawazo yake yaendane na ukweli kuhusu haki ya Mungu.
Toba ni kuyabadili mawazo kuhusu dhambi
Toba iliyo msingi wa imani ya kweli pia ni mabadiliko ya mawazo ya mtu kuhusu dhambi zake. Mpagani anaweza kuona dhambi zake (au maisha yake ya dhambi) siyo mbaya. Anaweza hata kuzipenda na kuzifurahia dhambi zake. Au anaweza kukubali kwamba dhambi zake nyingine ni mbaya, lakini siyo mbaya sana. Kama mtu huyo atatubu, anatakiwa kuwa na mabadiliko gani katika mawazo yake yahusuyo dhambi zake? Badala ya kuona dhambi zake kama kitu cha kuleta furaha au kitu kisicho kibaya sana, anatakiwa kuziona dhambi zake kama Mungu anavyoziona.
Mungu anaziona dhambi zake namna gani? Dhambi ni kitu kilichomtenganisha mwanadamu na Mungu. Dhambi zake zinamfanya kuwa adui wa Mungu. Dhambi zake zinamchafua kabisa na hana jinsi ya kujisafisha. Dhambi zake zinamfanya asiwe na njia ya kujipatanisha na Mungu. Dhambi zake zinamchukiza Mungu sana na kuileta ghadhabu ya Mungu na hukumu ya milele motoni. Mtu anayetubu kweli atayabadili mawazo yake kuhusu dhambi na kukubali kwamba mambo haya ni ya kweli.
Tokeo la toba
Mtu akitubu, yaani, akiyabadili mawazo yake kuhusu Mungu na kuhusu dhambi zake, basi, tokeo gani litafuata? Mtu akiona kwamba: 1) Ametengwa na Mungu mtakatifu; 2) Yeye ni adui wa Mungu; 3) Dhambi zake zimemchafua kabisa mbele ya Mungu mtakatifu; 4) Dhambi zake zinamfanya asiwe na njia ya kumkaribia Mungu wala kujipatanisha naye; 5) Dhambi zake zinamletea ghadhabu ya Mungu; 6) Mungu mwenye haki atamhukumu na kumwadhibu katika moto wa milele, jibu lake linatakiwa kuwa nini? Jibu linalohitajika litafanana na jibu la Isaya alipomwona Mungu na kugundua uchafu wa dhambi zake.
Tokeo la toba ni kuwa tayari kumwamini Yesu
Isaya 6:5 – “Ole wangu! Kwa maana nimepotea.”
Mtu asipojibu hivyo ina maana hajamwelewa Mungu jinsi alivyo na hajaziona dhambi zake kama Mungu anavyoziona. Ina maana hajatubu kweli kwa kuwa hajabadilisha mawazo yake kuhusu mambo hayo.
Mtu anayetubu, anayeyabadili mawazo yake kuhusu Mungu na kuhusu dhambi zake ili yapatane na ukweli wa Neno la Mungu, huyo sasa yu TAYARI kuisikia Injili na kuiweka imani yake katika Kristo. Mtu huyu aliyetubu kweli, je, ameokoka? Hapana. Hajaokolewa bado kwa sababu bado hajalitimiza sharti lile moja la wokovu la kumwamini Kristo! Lakini sasa mtu huyu ni TAYARI kuipokea Habari Njema ya Yesu na kuokolewa. Ndiyo maana tunasema kwamba toba si njia ya wokovu, lakini ni msingi wa imani inayookoa.
Tokeo la toba ni kukusudia kutotenda dhambi tena
Baada ya mtu kubadili mawazo yake kuhusu dhambi na kugundua ubaya na matokeo ya dhambi zake, mtu huyu hupaswa kufanya uamuzi moyoni. Kwa kawaida anatakiwa kukusudia moyoni mwake kutotenda dhambi tena. Kwa mfano, mtu anapotubu (yaani anabadili mawazo yake) kwamba kusema uongo kunamkasirisha Mungu, baada ya hapo anapaswa aamue asiendelee kusema uongo.
Tuangalie tofauti kati ya kukusudia kuacha kutenda dhambi na hali halisi ya kuacha kutenda dhambi. Ni muhimu tuone tofauti hiyo. Kuacha kutenda dhambi ina maana kweli kweli mtu huyu hatatenda dhambi tena katika maisha yake. Lakini, mtu akitubu na kubadili mawazo yake kuhusu kusema uongo, hivi kweli ataishi miaka mingi iliyobaki katika maisha yake bila kusema uongo tena? Hapana. Bila shaka atarudia dhambi hiyo ingawa amekusudia kutosema uongo tena. Tokeo moja la kutubu ni kukusudia kutorudia dhambi tena. Mtu anaweza kujaribiwa na kuanguka katika dhambi tena lakini kwa kuwa alitubu, ina maana, hataki kufanya dhambi tena. Kwa sababu mtu aliyetubu na kuelewa ubaya wa dhambi hataki kuendelea katika dhambi, akianguka, ataungama dhambi yake kwa Mungu na kuendelea na uamuzi ule ule wa kukusudia kutotenda dhambi.
Kwa mfano wakati mtu anatembea shambani, akiona panya kwenye njia, je, atageuka na kukimbia? Hapana. Kwa nini? Kwa sababu anajua panya huyu siyo hatari kwake. Lakini mtu huyu akiona nyoka kwenye njia atafanya nini? Atajitahadharisha. Aidha atageuka na kukimbia au atatumia kifaa fulani kumwua nyoka huyu. Kwa nini akimbie? Kwa sababu anajua nyoka ni hatari kwake na anamtambulisha kuwa adui wake. Kwa sababu hiyo, wanadamu hawataki hata kuwa karibu na nyoka.
Kwa mfano mwanamke akiingia katika nyumba yake na kuona nyoka mdogo, je, atasema, “Nitamwacha nyoka huyu kwa kuwa ni mdogo”? Hapana. Hata nyoka mdogo ni hatari na ni adui wa mwanadamu. Hawezi kumwacha nyumbani, lazima amwue.
Jinsi tunavyojisikia kuhusu nyoka ni sawa na jinsi mtu aliyetubu anavyojisikia kuhusu dhambi. Tunapaswa kuchukia dhambi zote, ziwe ndogo au ziwe kubwa. Tunapaswa kutambua dhambi kuwa adui yetu. Hatupaswi kuvumilia dhambi katika maisha yetu kwa kuwa tulishabadilisha mawazo yetu kuhusu ubaya na uharibifu wa dhambi. Yaani, tumegundua dhambi ni mbaya sana hadi inaleta kifo cha milele.
Kutubu ni hali endelevu
Jambo la mwisho tunalohitaji kujifunza ni kwamba toba ya kweli haiishi baada ya muda mfupi. Anayebadilisha mawazo yake kuhusu Mungu na dhambi anabaki na mawazo haya kwa maisha yake yote kama ametubu kweli. Kutubu ni uamuzi unaompeleka kwenye kumwamini Yesu lakini pia ni uamuzi wa kuendelea nao kila siku ya maisha yake. Ni vizuri kwa Wakristo kujikumbusha kila siku jinsi dhambi ilivyo mbaya na jinsi dhambi inavyomhuzunisha Mungu. Kama vile nyoka ni adui wetu maisha yetu yote, vilevile anayetubu kuhusu dhambi ajue dhambi ni adui wake kila siku ya maisha yake. Kwa sababu hiyo aliyetubu kweli kweli hawezi kuzoea dhambi kuwa jambo la kawaida katika maisha yake. Anaweza kutenda dhambi lakini atakusudia kutotenda dhambi tena kwa sababu alishabadilisha mawazo yake kuhusu ukweli wa dhambi. Na kwa msaada wa Roho Mtakatifu atafaulu zaidi na zaidi anapokua katika Kristo.