GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

WOKOVU - KAZI KUU YA MUNGU

- 10 -

Je, Yesu Alizifia Dhambi Zote?

Kabla hatujaendelea, tuhakikishe tunaelewa faida ya kifo cha Yesu kwa wote waliookolewa. Tuangalie tukio moja katika maisha ya mtu aliyeokolewa.

Mfano wa Benyamini aliyekufa kabla hajaungama

Benyamini alikuwa Mkristo aliyeokoka kweli lakini aliiba kalamu ya mtu. Kwa bahati mbaya alikufa mara moja baada ya tendo hilo na hakuweza kuungama dhambi hiyo kwa Mungu. Je, jambo gani litatokea atakaposimama mbele ya Mungu? Atahukumiwa na kutupwa katika ziwa la moto, au atapokelewa mbinguni?

Andika jibu lako:__________________________________________

Jibu lako litaonesha kama umeelewa vizuri kazi ambayo Yesu alimaliza msalabani kwa ajili ya wote waliookolewa naye. Ikiwa jibu lako ni kwamba atapokelewa mbinguni, ina maana umeelewa kazi ya Yesu msalabani. Lakini, kama umejibu kwamba atahukumiwa na kutupwa jehanamu, ina maana hujaelewa maana ya kifo cha Yesu.

Tunapookoka Yesu anachukua dhambi zote na kuzisafisha

Kumbuka Biblia inafundisha wakati Yesu alipokufa msalabani, Bwana Yesu alichukua au kusafisha dhambi zote na Mungu alimwadhibu Yesu kwa ajili ya dhambi zetu zote.

1 Yohana 1:7 – “Bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

1 Petro 2:24 – “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.”

Isaya 53:5-6 – “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; na BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote.”

Tunapookoka Mungu anasamehe dhambi zetu zote

Matokeo ya Bwana Yesu kuchukua juu yake mwenyewe makosa yetu yote na kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi hizo zote ni kwamba Mungu amesamehe makosa yetu yote.

Wakolosai 2:13 – “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote”

Tunapookoka Mungu anatangaza kuwa hatuwezi kuhukumiwa tena

Matokeo ya Mungu kusamehe dhambi zetu zote ni kwamba ye yote anayesamehewa dhambi zake zote hawezi kuadhibiwa tena kwa ajili ya dhambi zake. Kutokana na kazi ya Yesu msalabani, na imani ya mtu katika Yesu, Mungu anasamehe dhambi za mtu huyu na kutanganza hataadhibiwa tena. Tangazo hilo linatangazwa mara anapookoka. Mungu hasubiri mtu amalize maisha yake ili aweze kuona kama baadaye atafanya dhambi ambayo haitasamehewa. Mungu anatangaza mara moja akijua adhabu ya Yesu imelipia dhambi zote.

Warumi 8:1 – “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”

Mawazo ya uongo kuhusu kiasi cha dhambi Yesu alicholipia

Sasa tuangalie mawazo mengine yanayotaka kukanusha au kubishia mafundisho haya. Pia tuangalie mifano ambayo itatusaidia kuelewa kwamba Biblia inafundisha kwa uwazi kwamba wote waliookolewa hawataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao kwa kuwa Yesu alishasamehe dhambi zao zote hata kabla hawajazitenda zingine.

Wazo la uongo #1 – Yesu anasamehe tu dhambi zile zilizotendeka kabla mtu hajaokoka

Watu wengine wanasema wakati mtu anapookolewa, dhambi zile alizozitenda tayari zinasamehewa, lakini dhambi ambazo hajatenda bado haziwezi kusamehewa kwa kuwa bado hajazitenda.

Mfano unaofuata unaonesha kwamba inawezekana kwa dhambi kulipiwa na kusamehewa hata kabla dhambi hiyo yenyewe haijatendeka. Matokeo yake ni kwamba dhambi hiyo itakapokuja kutendeka, hakuna adhabu itakayotolewa.

Mfano: Uongozi wa kijiji ulitangaza kwamba kila mwanakijiji lazima awe na choo cha kuchimba kabla mwisho wa mwezi haujaisha. Tena walisema mwanzo wa mwezi unaofuata, viongozi watapitia kila nyumba na kukagua. Ye yote ambaye hana choo atawekwa ndani mpaka faini ya 10,000 tsh imelipwa. Mwisho wa mwezi ulipokaribia Petro alijikuta bado hajaanza kuchimba choo chake na ikaonekana atafeli kumaliza. Rafiki wa Petro, Mathayo, akaamua kwenda kwa uongozi wa kijiji na kuwataarifu kwamba Petro atashindwa kumaliza. Kwa sababu Mathayo hakutaka Petro kufungwa akaamua kumlipia faini yake hata kabla mwezi haujaisha; yaani kabla Petro hajakosea amri ya kijiji.

Wakati uongozi wa kijiji ulipitia nyumba ya Petro mwishoni mwa mwezi wakakuta hajamaliza choo chake. Je, waliweza kumfunga Petro ndani? Hapana. Kwa nini? Kwa sababu Mathayo alikuwa ameshamlipia Petro faini yake hata kabla hajaingia kwenye kosa.

Vivyo hivyo Bwana wetu Yesu Kristo aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi zetu msalabani hata kabla hatujazaliwa na kutenda hata dhambi moja. Dhambi zetu zote bado zilikuwa katika siku zijazo wakati Yesu alisulubishwa, yaani dhambi zetu ambazo tulitenda kabla hatujaokolewa na dhambi zetu tulizotenda baada ya kuokolewa. Dhambi zote hizo zilisamehewa zaidi ya miaka 2000 iliyopita wakati Yesu aliadhibiwa msalabani.

Kwa sababu dhambi zote ziliadhibiwa msalabani, Mungu hataadhibu ye yote anayemwamini Yesu na kuokolewa. Hataadhibu dhambi zilizotendeka kabla mtu hajaokoka na hataadhibu dhambi za mtu zilizotendeka baada ya kuokoka kwa kuwa alishaziadhibu zote katika Yesu.

Wazo la uongo #2 – Lazima mtu aungame dhambi zake baada ya kuokoka au hatasamehewa na atalazimika kuadhibiwa baada ya kufa kwake.

Watu wengine wanasema, ingawa Yesu alifia dhambi zote, hatasamehe dhambi ambazo mtu aliyeokolewa hajaziungama. Na mtu akikosa kuungama dhambi fulani atahukumiwa milele kwa ajili ya dhambi hizo.

Mfano unaofuata unaonesha wakati dhambi au kosa limeshaadhibiwa, isingekuwa haki mtu huyu aadhibiwe tena kwa kosa lile lile.

Patriki aliiba kuku wa jirani yake. Tendo hilo lilikuwa kinyume na sheria na alilazimika kuadhibiwa alipokamatwa. Uongozi wa kijiji chake uliamua Patriki alipe faini ya 10,000 tsh kwa ajili ya kosa la kuiba kuku huyo. Lakini Petro hakuwa na 10,000 tsh kwa ajili ya kulipa. Hivyo kesho yake Samweli, rafiki wa Petro, aliamua kwenda kumlipia Petro deni lake lote. Lakini siku iliyofuata viongozi wa kijiji walirudi kwa Petro na kumdai 10,000 tsh kwa ajili ya kuiba kuku yule. Je, viongozi wana haki kumdai Petro kwa mara ya pili wakati deni lake lilishalipiwa kwa kosa hilo hilo? Hapana. Baada ya faini ya Petro kulipiwa mara ya kwanza, Petro alikuwa hana hatia tena. Kumlazimisha kulipa kwa mara ya pili kungekuwa kutomtendea haki.

Bwana Yesu Kristo alilipia deni la dhambi zote la watu wote waliomwamini na kuokolewa. Yesu aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi zote na Mungu aliridhika na malipo yake. Je, Mungu mwenye haki anaweza kumwadhibu mtu kwa ajili ya dhambi ambazo zimeshaadhibiwa kupitia Yesu Kristo? Hapana. Kumwadhibu mtu kwa dhambi ambazo Yesu alishaadhibiwa kungekuwa kuadhibu dhambi zile zile mara mbili. Kufanya hivyo kusingekuwa sahihi na Mungu mwenye haki hawezi kufanya hivyo. Kwa kuwa dhambi inaweza kulipiwa mara moja tu, na kwa kuwa Biblia inafundisha dhambi zetu zililipiwa na Yesu msalabani, mtu aliyeokoka hawezi kuadhibiwa tena kwa kuwa dhambi zake zilishalipiwa. Ndiyo maana tunasoma katika Warumi 8:1, “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”

Isitoshe, haiwezekani mtu kukumbuka na kuungama dhambi zake zote kwa maana ya kutaja kila dhambi. Watu wengine wanaokoka katika uzee wao. Je, kweli wanaweza kukumbuka kila dhambi waliyoitenda ndani ya maisha yao yote ili waziungame? Haiwezekani. Dhambi zetu ni nyingi mno na Mungu hategemei tuweze kukumbuka kila moja. Hata hivyo ni kawaida ya wanadamu kutotambua kila dhambi wanayotenda. Mtu atawezaje kukumbuka dhambi ambayo hajui aliitenda? Hawezi. Ni kweli Mungu anataka tuungame kila dhambi tunayotambua na kukumbuka lakini kutoadhibiwa kwetu hakutegemei uwezo wetu wa kukumbuka kila dhambi na kuiungama. Mtu anapookoka anakiri dhambi zake kwa ujumla na Mungu anazisamehe kwa ujumla. Tena anamsamehe hata dhambi ambazo hajazitenda bado, yaani dhambi ambazo atazitenda baadaye katika maisha yake ya kikristo. Ingekuwa ni kweli tunapaswa kuungama kila dhambi kwa kuitaja, wote tungeadhibiwa na kuhukumiwa kwa sababu wote tungesahau angalau dhambi moja na hukumu ya dhambi moja tu ni mauti ya milele.

Kutafakari zaidi kuhusu mawazo haya ya uongo
​

Mchoro unaofuata unaonesha mifano mbalimbali ya jinsi Mungu anavyoweza kufikiria msamaha wa dhambi. Mifano mingine ni sahihi kulingana na mafundisho ya Neno la Mungu na mifano mingine ni ya uongo. Katika michoro hii mstari wa chini ni mfano wa maisha ya mtu, “x” ni mfano wa dhambi zake ambazo hazijasamehewa, na mchoro wa msalaba unaonesha wakati ambao mtu huyu aliokolewa katika maisha yake.
Picture
Mchoro #9 – Huu ni mfano wa jinsi ambavyo maisha ya mtu yangeonekana machoni pa Mungu kama Mungu hajasamehe dhambi zake hata moja.
Picture
Mchoro #10 – Huu ni mfano wa mtu ambaye Mungu alisamehe dhambi zake zilizotendeka kabla hajaokoka (wazo la uongo).
Picture
Mchoro #11 – Huu ni mfano wa mtu aliyeokoka na Mungu alisamehe dhambi zake zote kasoro moja mwishoni mwa maisha yake ambayo hakupata nafasi ya kuungama (wazo la uongo).
Picture
Mchoro #12 – Huu ni mfano wa mtu aliyeokoka na Mungu alisamehe dhambi zake zote.

Mchoro #10 hapo juu unaonesha maisha ya mtu ambaye Yesu aliadhibiwa kwa ajili yake na Yesu aliondoa dhambi zote zilizotendeka na mtu huyu kabla hajaokoka. Tumaini la mtu huyu ni kwamba dhambi anazozitenda baada ya kuokoka zitasamehewa wakati anapoungama dhambi zake kwa Mungu njiani. Lakini tunahitaji kuuliza swali moja: Kama Yesu aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi zilizotendwa na mtu huyu kabla hajaokoka, je, nani ataadhibiwa kwa ajili ya dhambi alizotenda baada ya kuokoka?

Watu wengine wanasema mtu akiungama dhambi zake kwa Mungu, Mungu atafuta dhambi zake na kumsamehe. Je, kuungama kunaweza kuondoa dhambi za mtu? Biblia inasema nini? Katika Waebrenia 9:22 tunasoma pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo la dhambi. Maana yake nini “kumwaga damu”? Yesu angekata mguu au mkono wake na kumwaga damu, je, damu ile ingeweza kuleta msamaha wa dhambi? Hapana. Maana ya kumwaga damu ni mauti. Mauti ndiyo malipo ya dhambi (Rum 6:23). Wakati mtu anaungama dhambi zake, nani anakufa? Hakuna mtu. Yesu asingeondoa dhambi zote wakati alipokufa msalabani, kitu gani kingine kingeweza kuondoa dhambi? Hakuna.

Kama Yesu hakuondoa dhambi zote msalabani, basi Yesu hakumaliza malipo ya dhambi zote. Atakuwa amelipa sehemu ya malipo tu. Na kama hali hii ni kweli nani atamaliza malipo yale ya dhambi ambayo Yesu hakumaliza? Jibu ni yule aliyezitenda. Atahitaji kuadhibiwa milele katika ziwa la moto ingawa katika wazo hilo la uongo Yesu aliadhibiwa kwa baadhi ya dhambi zake.

Tunajua kwa hakika kwamba Mungu ataadhibu dhambi zote. Kama Yesu aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi za watu zilizotendeka kabla hawajaokoka, nani ataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao zilizotendeka baada ya kuokoka? Jibu tena ni yule aliyezitenda, tena atahitaji kuadhibiwa milele kwa kuwa ndiyo malipo ya dhambi hata moja.

Kama Yesu hakuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zote na kama hakuondoa dhambi zote msalabani, watu wote wataadhibiwa kwa dhambi zao ambazo Yesu aliziachilia. Na kama hali hii ni kweli, kumbe hatuna tumaini la kuokolewa.

Mchoro #11 hapo juu unaonesha maisha ya mtu ambaye Yesu aliadhibiwa kwa ajili yake na Yesu aliondoa dhambi zake zote kasoro moja aliyotenda katika dakika zake za mwisho duniani. Kwa sababu alikufa ghafula, hakupata nafasi ya kuungama dhambi hiyo ya mwisho. Tuulize swali letu tena: Ikiwa Yesu aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake zote kasoro moja, nani ataadhibiwa kwa ajili ya dhambi hiyo moja iliyobaki? Jibu tena ni yule aliyeitenda. Lakini mfano huu ni wa uongo kwa sababu ukweli ni kwamba Yesu aliadhibiwa tayari kwa ajili ya dhambi zote za kila mtu anayemwamini Yesu.

Mchoro #12 hapo juu unaonesha maisha ya mtu ambaye Yesu aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake zote. Mtu huyu amesamehewa dhambi zake zote. Kwa sababu dhambi zake zote zimesamehewa, mtu huyu hawezi kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake. Mtu huyu kweli ameokolewa.

Kama huamini kwamba Yesu alikufa na kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zako zote wakati ukweli ni kwamba ameondoa na kusamehe dhambi zako zote, inakubidi kuchimba zaidi katika kitabu hiki na Neno la Mungu mpaka wakati utakapoelewa na kuamni ukweli huo unaofundishwa na Biblia. Kama Yesu hakuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zako zote wakati alipokufa msalabani, Mungu atalazimika kukuhukumu na kukuadhibu kwa dhambi zile ambazo Yesu hajakulipia (Kumbuka Mungu ni mwenye haki na ni lazima aadhibu dhambi zote). Hivyo kama Yesu alipokea adhabu yako ya dhambi zote kasoro moja, basi wewe utaadhibiwa milele kwa dhambi ile moja iliyobaki. Je, adhabu ya hata dhambi moja ni nini? Ni mauti ya milele; ni hali ya kutenganishwa na Mungu milele na milele katika ziwa la moto. Kwa hiyo, kama Yesu hajakulipia dhambi zako zote na kuziondoa, basi hakuna wokovu na utaangamizwa kwa ajili ya dhambi zako.

Lakini usihangaike! Biblia inafundisha kweli kwamba Yesu alikuja duniani ili aokoe wenye dhambi wasiadhibiwe kwa ajili ya dhambi zao. Mtu akisema Yesu alisamehe baadhi ya dhambi tu, mtu huyu ni mwongo na haelewi mafundisho ya Neno la Mungu. Ingemaanisha kwamba Yesu hakutimiza kusudi lake la kuja duniani. Zaidi mtu akisema hivyo ina maana kifo cha Yesu hakina kazi kwa sababu watu wote bado wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao ambazo hazikulipiwa. Mawazo kama hayo hupuuza kazi kubwa ambayo Yesu alifanya msalabani. Mawazo kama hayo siyo sahihi, tena ni ya uongo.

Hoja ya uongo kwamba mafundisho haya yataruhusu Wakristo kutenda dhambi

Lakini wengine wanaogopa kufundisha mawazo ya kibiblia kwamba mtu aliyeokoka amesamehewa dhambi zake zote, ikiwa ni pamoja na zile alizotenda tayari na hata zile ambazo atatenda baadaye. Wanaogopa Mkristo huyu atazidi kutenda dhambi bila kujali akifundishwa hivyo. Mtume Paulo anasema, “Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (Rum 6:12). Yaani, Mkristo wa kweli hawezi kuwa na tabia ya namna hiyo. Kumbuka mwanzoni mwa kitabu hicho tulisema kwamba kila mtu lazima achague yule atakayemtumikia. Mkristo ni mtu aliyeamua kumtumikia Mungu na kuachana na dhambi. Kuendelea katika dhambi bila kujali kusingeonesha shukrani yo yote kwa ajili ya wokovu huu wa ajabu unaopatikana katika Yesu. Tubaki katika mafundisho ya kweli ya Neno la Mungu na tubaki katika hali ya kumwabudu, kumtumikia, na kumshukuru Mungu tukiachana na dhambi.
 
Kwa nini wengine wataadhibiwa ikiwa Yesu alifia dhambi zote?

Pengine mafundisho haya yatakuwa yamezalisha swali kwako. Labda utauliza, “Je, kama Yesu aliadhibiwa kwa ajili ya dhambi za walimwengu wote, kwa nini wengine wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao, hasa kama siyo haki kuadhibu dhambi zile mara mbili?” Hilo ni swali zuri linaloonesha unafuata kwa ukaribu somo letu.

Jibu letu la kwanza ni kusema tunaamini hivyo kwa sababu Biblia inafundisha hivyo. Lazima tubaki katika mafundisho ya Biblia. Biblia inafundisha kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya kila mwanadamu na zaidi alikufa kwa ajili ya dhambi zote za kila mwanadamu. Mistari ya Biblia ni mingi sana inayofundisha mafundisho hayo (kwa mfano: Yn 3:16, Ebr 2:9, 1 Tim 2:4-6, 4:10, 1 Yoh 2:2 n.k.). Vilevile Biblia inafundisha wengine watahukumiwa kwenye ziwa la moto. Hivyo tunaamini hali zote mbili ni kweli.

Inawezekanaje? Jibu ni kwamba wengine wanakataa malipo ya Yesu na wanataka walipe wenyewe. Unaweza kumlipia mtu deni lake, lakini akikataa na kutaka kulipa mara ya pili mwenyewe huwezi kumzuia. Maana yake ni kwamba Mungu aliandaa njia kwa ajili ya watu kuondolewa dhambi zao na kusamehewa. Njia ile ni kumwamini Yesu Kristo na kazi yake msalabani. Mungu alimwadhibu Yesu kwa ajili ya wote. Lakini ni lazima kila mtu apokee neema hiyo kutoka kwa Mungu kwa njia ya kumwamini Yesu. Kila asiyeamini anatangaza hataki Yesu kubeba dhambi zake na pia anatangaza anataka abebe mwenyewe. Kwa mfano baba wa nyumba anaweza kufanya kazi nyingi ili chakula kipatikane kwa familia yake. Kazi imetendeka na chakula kimepatikana. Lakini mwingine katika familia anaweza kukataa kula chakula kile. Hivyo, ingawa chakula kiliandaliwa, anayekataa chakula hicho atahitaji kutafuta chakula chake mwenyewe.
​
Vivyo hivyo Mungu aliandaa njia ya msamaha kwa kumwadhibu mwana wake Yesu Kristo. Lakini kuna sharti kwa kila mtu ili afaidike na msamaha ule; sharti lile ni imani katika Yesu.

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 11
Proudly powered by Weebly