GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

UINJILISTI UFANYAO KAZI

- 9 -

Namna ya Kuwaendea Watu

Mara nyingi sana utasikia makanisa yakihimiza watu kueneza Injili lakini hawawafundishi jinsi ya kufanya. Kukosa elimu na ujuzi hufanya watu kushindwa katika kazi ya uinjilisti na mara nyingine huleta matokeo ya kugombana badala ya kushuhudia. Naamini kwamba kuna njia chache, ambazo tukizijua, zinaweza kutusaidia jinsi ya kuwaendea watu ili wapate kutusikiliza vizuri.

Kwanza kabisa, ni kurudia yale tuliyojifunza huko nyuma kwamba mwinjilisti ni mwenezaji wa upendo wa Mungu. Kutokana na hali hii, ni lazima mwinjilisti aongee kwa upendo na upole anapoongea na wote anaowaendea. Nimekuta mara nyingine watu wakishafahamu kuwa unataka kuwashuhudia wanachemka kusudi wajikinge na maneno yako wakitetea hali yao au kanisa lao. Njia ya kufaulu katika kushuhudia watu hawa ni kutochemka wewe mwenyewe na kuwasikiliza kwa upendo na upole. Wasikilizaji watatulia kulingana na jinsi uanvyowaonesha upendo. Hata wasikilizaji wengine watakuheshimu kutokana na hali yako ya upendo wakati mtu unayemshuhudia anakataa ujumbe wako kwa hasira. Lakini kumbuka tulijifunza kutobishana kamwe.

Ninapenda sana kutumia neno “mwingilio” katika kueleza namna ya kufanya uinjilisti. Mwingilio unatumika pale unapozungumza na mtu katika hali ya kujenga urafiki na nafasi inapatikana kubadili mazungumzo ili uanze kumshuhudia Kristo (mara nyingine bila hata msikilizaji kufahamu). Hii ni njia bora niliyoigundua ya kumfanya mtu awe na hamu kuisikia Injili. Kufanya hivyo humfanya msikilizaji asijisikie kwamba “anahubiriwa”. Miingilio ni mingi sana na hubadilika kulingana na hali ya msikilizaji na mazingira yake. Faida ya kuitumia miingilio ni jinsi inavyokuwezesha kuyalenga hasa mahitaji na moyo wa msikilizaji kutoka mwanzo wa mazungumzo yako hadi mwisho wakati unapomshudhudia Injili ya Yesu.

Nimeona mafanikio makubwa kwa wachungaji na wanafunzi wa chuo cha uchungaji (Tanzania Grace Bible Institute) wakitumia njia hii nilipowafundisha mwaka 1991-1994. Wanafunzi, na mimi mwenyewe, tulishangaa kuona katika uinjilisti wa wanafunzi, wastani wa mafanikio yao ulikuwa yapata 20-25%. Yaani, kati ya watu wanne au watano walioshuhudiwa na wanafunzi kwa taratibu hii mmoja alikata shauri! Ni matokeo ya ajabu! Tukumbuke kwamba mbinu na ujuzi hauwezi kuokoa bali Roho Mtakatifu huokoa. Lakini ni wajibu wetu kujifunza kutumia njia zilizo bora ili Neno La Mungu lipate kusikika vizuri, maana, “Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rum 10:17).

Watu Watapataje kuamini tukikosea namna ya kuwaendea na kuwahamasisha wausikilize ujumbe wetu wenye maana? Basi tujifunze njia mbalimbali za miingilio zinazoweza kutumiwa na watu wote.
 
MIINGILIO YA INJILI

1. Njia ya kundi fulani.

Ni vizuri kuwaambia watu kwamba wewe ni mmojawapo wa kundi fulani kama umoja wa vijana wa kanisa, au mwanafunzi wa shule fulani, n.k. Kuwaelezea watu hivyo itawasaidia kufahamu kwamba huna makusudi mabaya. Vilevile hawatafikiri wewe ni kichaa anayebisha hodi milangoni mwa watu bila sababu. Watakaposikia wewe ni wa kundi fulani ndipo watafikiri bila shaka ujumbe wako ni wa muhimu kwa kuwa wengi wanashughulika nao. Halafu wenyewe wanaweza kuwa na hamu kujua ni nini chenye umuhimu wa kiasi cha kukufikisha kwao. Hapo ndipo utakapopata nafasi yako ya kuelezea ujumbe wako ulio muhimu sana.

2. Njia ya maandiko.

Unaweza kutembea na vipeperushi au vitabu vya kuuza. Uvioneshe wazi na kuwaelezea watu kwamba umewaletea maandiko mazuri ya kuwasaidia katika maisha yao. Maandiko haya yanaweza kufundisha kusudi la Mungu kwa ajili wanadamu na njia ya kwenda mbinguni.

3. Njia ya ushuhuda wako.

Baada ya kuandaa ushuhuda wako kwa makini, unaweza kuutumia kuingiza Injili. Kwa mfano unaweza kusalimiana na watu na baada ya kufahamiana nao ukasema, “Je, naweza kupata muda mfupi nikuelezee juu ya kitu fulani kilichonitokea ambacho kitakupendeza?” Au, “Ningependa kukuambia kuhusu kitu kilichonitokea ambacho ni muhimu kuliko vyote maishani mwangu.”

4. Njia ya watoto.

Mara nyingi watoto wanakuwepo pamoja na wazazi wakati unapowatembelea nyumbani mwao. Utawapendeza wazazi unapoonesha furaha kwa watoto na kuwajali. Kumjali mtoto ni sawa na kuwathamini wazazi wake. Unaweza kuwasifu watoto na kuwapongeza wazazi kwa kazi ngumu ya kulea watoto. Halafu utumie tamko hilo kama mwingilio ukieleza jinsi tunavyozaa watoto na kuwafundisha ili wafanane na wazazi, na ndivyo ilivyo kwa Mungu.

5. Njia ya habari.

Kwa kuzifahamu habari za dunia au za eneo lile unalolitembelea, unaweza kuzitumia habari hizo kama mwingilio wa Injili katika kushuhudia kwako. Kwa mfano unaweza kuzitumia habari za hali ya hewa, vita, mateso, njaa, ajali za magari na ndege, au uvumbuzi mpya. Yote haya yanaweza kutumiwa kuingiza Injili na kuonesha jinsi Injili ni ya muhimu na ya kisasa kulingana na hali ya dunia ilivyo. Hata habari za kanisa, siasa, na wevi zinaweza kutumiwa kama mwingilio.

6. Njia ya dhehebu.

Unaweza kuongea kuhusu madhehebu, jinsi yalivyo mengi siku hizi, na jinsi wote wanavyotafuta ukweli wa Mungu na njia ya kufikia kwake. Au, unaweza kueleza kwamba msingi wa imani ni Neno la Mungu, na kwa sababu hiyo ni bora kuchunguza ujumbe wa Mungu katika Neno lake kuliko kuongea mambo ya kidhehebu. Au, unaweza kueleza kwamba wewe ni wa dhehebu fulani nawe umegundua Injili ya Mungu ambayo siyo ya dhehebu lo lote bali ni ya watu wote.
​
7. Njia ya kanisa.

Kwa kutumia jina la kanisa lako la mahali unaweza kuvuta watu kutaka kujua zaidi juu ya imani yake. Hasa kama kanisa ni jipya au mnafanya ujenzi katika eneo fulani, hali hii itawaongeza hamu kusikia juu ya imani ya kanisa hilo. Waelewe kuwa katika kanisa lako mmeona umuhimu wa kuwatembelea watu na kuzungumza nao kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu.
 
8. Njia ya uchunguzi kuhusu jinsi watu wanavyosoma Biblia.

Unaweza kuzunguka ukikusanya takwimu kama anayefanya sensa. Unaweza kuuliza: (1) Kama mtu anayo Biblia au sehemu ya Biblia? (2) Kama anaisoma? (3) Kwa taratibu gani anaisoma? (4) Kama anayaelewa anayoyasoma? (5) Kama katika kusoma Biblia ameona na kuyaelewa makusudi ya Mungu kwa wanadamu? Maswali kama haya yaweza kuwaingiza katika Injili kwa urahisi.

9. Njia ya kutumia siku ya sikukuu.

Sikukuu ni siku ya kusherekea kitu fulani. Kwa hiyo kuna maana muhimu kwa siku yenyewe ambayo maana hiyo inaweza kutumiwa kuingizia Injili. Krismasi na Pasaka ni rahisi kutumia upande wa uinjilisti lakini hata nyingine zinaweza kutumiwa kwa mfano: siku ya uhuru, mashujaa, wafanyakazi, muungano, mwaka mpya, wakulima, na hata sikukuu za dini nyingine.

Kwa kuyaangalia mapendekezo yaliyotajwa hapo juu unaweza kuona kwamba njia za kuingizia Injili ni nyingi sana na unapaswa kujizoeza kuzitumia wewe mwenyewe.
Wakati huu nakushauri ujibu maswali yanayofuata halafu ujitahidi kuzunguka na kuwashuhudia watu ukitumia maarifa uliyojifunza hadi hapa katika kitabu hicho. Umtegemee Mungu kwa nguvu na ujasiri na kwa mafanikio yo yote anayokusudia Yeye.
 
MASWALI NA MAJADILIANO


  1. Neno “Mwingilio” lina maana gani katika uinjilisti?
  2. Kwa nini ni muhimu kujifunza namna ya kuwaendea watu?
  3. Mtu akichemka unapomwendea ni bora kufanya nini?
  4. Kama utatumia mwingilio wa ushuhuda wako, unaweza kutumia maneno gani? Toa mfano.
  5. Toa mfano wa mwingilio kwa habari za: (1) Ajali ya magari; (2) Hali ya hewa; na (3) Uvumbuzi mpya.

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 10
Proudly powered by Weebly