GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

UINJILISTI UFANYAO KAZI

- 8 -

Vizuizi vya Kuamini

Katika kufanya uinjilisti wa mtu kwa mtu ni lazima utakutana na vizuizi mbalimbali. Maana, tulijifunza kazi hiyo ni ya kiroho na mpinzani wa mambo ya kiroho yupo. 2 Korintho 10:3-5 inasema, “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo.” Shetani hawezi kutulia na kuona wafuasi wake wanavuliwa bila kuinuka na kufanya bidii kuzuia mafanikio katika uinjilisti wako. Ndiyo maana ni lazima kazi ya uinjilisti ifanyike kwa kumtegemea Roho Mtakatifu, nguvu zake za kuokoa, na uwezo wake wa kumshinda adui yule. Katika somo hili tunataka kujifunza jinsi gani Shetani anavyoleta vizuizi ili watu wasiamini. Kazi yetu ni kutumia silaha za roho ili tushinde vizuizi vya Shetani na watu wapate kumtii na kumkiri Kristo kama Bwana na Mwokozi wao.

Sasa tuangalie vizuizi vikubwa vitano halafu tutaweza kuorodhesha vingine tunavyokutana navyo tukiwa kwenye uinjilisti.

1. “Ningependa kuokolewa, lakini nafahamu kwa hakika kwamba nitashindwa kuishi maisha mazuri ya Mkristo wa kweli.”

Mara nyingi mtu unayemshuhudia hawezi kukitamka kizuizi hicho wazi. Anakataa kuamini lakini hasemi kwa nini. Ukigundua hicho ndicho kizuizi kwake ufanye nini? Kwanza ni vizuri kwa kuwa mtu huyu ameshafahamu Mungu hutaka watu kubadilika na kuwa wazuri. Ingawa Mungu huwapokea kama walivyo, anataka kuwafanya wawe wazuri ili wafanane na Yesu Kristo! Tatizo la mtu huyu ni jinsi ambavyo anaona atashindwa kubadilika akijua uwezo wake ni mdogo. Anachokosea ni kwamba hajagundua hakuna anayeweza kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kwa uwezo wake mwenyewe. Kushinda na kubadilika kunategemea uwezo wa Mungu na kuingiliwa na Roho Mtakatifu. Mtu huyu astahili kufundishwa juu ya kazi ya Roho Mtakatifu na jinsi Mungu anavyowezesha Mkristo kubadilika baada ya kuokolewa akianza maisha ya kumfuata Kristo.

2. “Marafiki na jamaa zangu watanicheka na kunidharau nikiwaambia nimeamini na kuokolewa.”

Yesu Kristo aliyajua mawazo haya alipowaambia wanafunzi wake katika Luka 9:26, “Kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.”

Kizuizi hiki kinaweza kupinduliwa kwa kumweleza msikilizaji mambo yafuatayo:

  1. Kukubaliwa na Mungu ni jambo la muhimu kuliko kukubaliwa na wanadamu. Baada ya miaka 50 au 100 kibali cha nani kitakuwa muhimu zaidi?
  2. Watu wasiomfahamu Kristo kama Mwokozi wao daima watamdharau, maana hata Kristo alidharauliwa. Vilevile Biblia inasema kwamba ujumbe wa Injili ni upuuzi kwa watu wa dunia (1 Kor 2:14) kwa sababu hawauelewi.
  3. Nafuu yeye aokolewe kwa sababu atakufa peke yake na atasimama mbele za Mungu peke yake. Atakapobadilishwa, kama Mkristo, ndipo atapata nguvu za kuwashuhudia wale wanaomcheka ili nao pia wapate kuamini badala ya kupotea. Bora asiongozwe na mtu aliyepotea kuhusu mambo ya kiroho.

3. “Mimi siyo mtu mbaya na siamini kwamba Mungu atanihukumu kama unavyoeleza.”

Mtu huyu ameziamini akili zake na mawazo yake kuliko Neno la Mungu. Kumpokea Kristo hakuji kwa kujiamini bali ni kwa kumwamini Yesu Kristo na Neno Lake. Mara nyingi kizuizi hicho utakisikia kwa wasomi na wenye elimu. Kristo mwenyewe alisema, “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani” (Yn 5:24). Lazima mtu huyu akubali Neno la Mungu zima ni la kweli na kwamba hawezi kuchagua anachotaka kuamini na kuacha asichotaka.

4. “Mimi nimefanya dhambi nyingi na hata ile ‘dhambi isiyoweza kusamehewa’.”

Mtu huyu huhitaji kufafanuliwa kwamba “dhambi isiyoweza kusamehewa” ilikuwa dhambi ya kusema uwezo na ishara za Kristo ziliwezeshwa na Shetani badala ya kuwezeshwa na Roho Mtakatifu. Yaani, ni kumwasi Kristo. Leo anayekataa kumwamini Kristo anamwasi Kristo na akifanya hivyo hadi kufa atapotea milele. Lakini ye yote anayemwamini na kumpokea Kristo anasamehewa dhambi zake zote na anapata kuwa kiumbe kipya (2 Kor 5:17). Hakuna dhambi isiyosamehewa isipokuwa kutoamini.

Soma Zaburi 103:3, 10, 12: “Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, wala kutulipia kwa kadiri ya maovu yetu. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.”
 
VIZUIZI VINGINE VINAVYOSUMBUA

Vizuizi vingine vipo vingi. Angalia vilivyotajwa hapo chini na jaribu kuandika jinsi ya kuvishughulikia na kuvijibu:

  1. Unaposhuhudia, mtu mmoja hadi mwingine anaongezeka mpaka umati umepatikana. Hivyo, msikilizaji wako anakosa kusikiliza vizuri na kuamini kwa kuogopa wenzake waliokusanyika.
  2. Mtu unayemshuhudia ana shughuli nyingi. Unapoendelea kueleza Injili anachunguza saa yake na kufikiri kuhusu mambo mengine hata kuinuka na kufanya mengine badala ya kufikiria maana ya ujumbe wako.
  3. Mtu ameisikia Injili lakini ni jambo geni kwake. Hajaifikiria vya kutosha na hajakomaa katika mawazo yake ili aamini.
  4. Mtu anayaogopa mabadiliko magumu ya kuachana na maisha yake ya zamani na pengine hata marafiki zake na familia yake.
  5. Mtu amezaliwa katika dini ya wazazi wake na hataki kuiacha dini yake wala kuamini ujumbe wako ingawa dini yake inakataa wokovu duniani.
  6. Jaribu kutaja na vizuizi vingine unavyovijua wewe.
 
MASWALI NA MAJADILIANO

  1. Kwa nini tunaweza kuvikuta vizuizi tunapofanya kazi ya uinjilisti?
  2. Mtu anayeogopa kuchekwa anaweza kusaidiwaje na hofu yake?
  3. Je, mtu anayekataa kuamini ujumbe wa Neno la Mungu anawezaje kushuhudiwa?

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 9
Proudly powered by Weebly