GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

UINJILISTI UFANYAO KAZI

- 6 -

Njia ya Kushuhudia

Mpaka sasa tumejifunza kuhusu maandalizi ya mwinjilisti na ujumbe tunaoshuhudia. Vilevile tumejifunza jinsi ya kutumia ushuhuda wetu kuongeza nguvu katika uinjilisti wetu na mwishoni tumeangalia vifaa vya uinjilisti wa mtu kwa mtu. Kwa hiyo sasa tunastahili kuchunguza utendaji wa uinjilisti wenyewe. Yaani jinsi ya kushuhudia mtu mmoja mmoja au nyumba kwa nyumba. Tutaangalia somo hili kwa sehemu tatu: (1) Unapoenda kushuhudia na njiani; (2) Unapomfikia mtu mwenyewe na kumshuhudia; na (3) Unapotaka kumaliza na kuachana na mtu uliyemshuhudia.
 
KWENDA KUSHUHUDIA

Katika siku ambayo unataka kuondoka kwenda kuwashuhudia watu fulani kuna mambo mbalimbali ya kukumbuka.

1. Panga timu yako na eneo utakaloendea.

Mkutane kanisani au nyumbani mwa mtu mmoja kati ya timu yako ya uinjilisti. Mwe watu wawili au watatu, mkiwa zaidi mtamwogofya msikilizaji. Pia, mkiwa zaidi ya jinsia moja, lazima wanaume wawe wawili au wanawake wawe wawili kuondoa mawazo mabaya ya watu (yaani msiende mwanaume mmoja na mwanamke mmoja kama siyo mume na mke wake). Timu ya namna hiyo inaweza kukutana na wanawake au wanaume. Ikiwa timu yako ni watu wa jinsia moja basi mlenge hasa watu wa jinsia yenu (yaani kiume kwa kiume na kike kwa kike).

Timu yenu inapaswa kupanga maeneo mnayolenga kushuhudia ili juma linalofuata mweze kuanza huko na kuendelea hadi mmalize sehemu yote mliyoipanga. Ni vizuri kupanga maeneo mtakayofululiza mpaka umemaliza kijiji au hata mji. Vilevile, mkiwa na mpango itasaidia timu nyingine kulenga maeneo bila kuingiliana au kushindana nanyi.
  
2. Lazima timu iombe pamoja kabla ya kuwaendea watu.

Kwanza timu yenu inapaswa kujiombea, mkimwomba Mungu kuwatumia kama vyombo safi kueneza Injili. Pili, timu yenu inapaswa kuwaombea wale watakaosikiliza Injili. Kazi ya uinjilisti ni ya kiroho na kuianzisha kwa maombi ni muhimu. Kufanya hivyo kunamkabidhi Mungu kazi yake ya kuokoa roho za watu kama apendavyo Yeye. Pia, kunatukumbusha nguvu zetu zatoka wapi ili tumtegemee Mungu kwa mafanikio.

3. Njiani timu iamue nani atakuwa msemaji na nani atakuwa mshiriki mkimya.

Msiingie nyumba ya mtu bila kufanya maelewano hayo, ingawa mnaweza kuwa na ishara kama kutikisa kichwa au macho kumaanisha mwenzako aanze pale ulipofikia. Bila kufanya hivyo mnaweza kuwa na mvutano katika kueleza Injili mpaka ujumbe hauendi sawa na msikilizaji anatoka bila kuelewa kitu cho chote.

4. Mnapokaribia nyumba ya mtu, au mtu mwenyewe, chunguza kwa siri mazingira ili mpate kugundua ni mtu wa aina gani.

Kufanya hivyo itawasaidia kuanzisha mazunguzo ya kirafiki naye. Vilevile itawasaidia kupata “mwingilio” wa kueleza Injili. Kwa kadiri mnavyomfahamu mtu ndivyo mnavyoweza kumlenga katika mahitaji yake hasa. Kwa mfano akiwa na sanamu ya bikira Mariamu mtagundua dhehebu na imani yake ilivyo, kwa kuona picha za nyumba yake mtafahamu kilicho muhimu kwake, na kwa kunusa harufu ya pombe mtajua ni mtu anayeshiriki au kukoroga pombe, n.k. Hayo yote yatawasaidia kuanzisha mazungumzo yenu.
 
UNAPOKUTANA NA MTU MWENYEWE

Jinsi tunavyokutana na watu na kuongea nao kunaweza kufanya watu wawe na hamu ya kusikia ujumbe wetu hadi kuamini au kunaweza kufunga masikio yao na kuwafanya kukataa ujumbe wetu. Kwa hiyo ni muhimu sana tuangalie tunavyoongea nao. Hapo chini ni mapendekezo machache.
 
 1. Onesha furaha na tabasamu.

Ni wazi kwamba mtu aliyechangamka anapendwa na watu kuliko anayeonesha kwamba huduma hiyo ni huzuni na mzigo kwake. Basi, onesha kwa sura yako kwamba ujumbe wako ni Habari Njema.

2. Ujitambulishe na upate kumfahamu msikilizaji kwa jina pia.

Hiyo itakusaidia kuongea naye kwa kutumia jina lake. Pia, utakapojitambulisha utaanza kuondoa wasiwasi wo wote alio nao kuhusu wewe. Maana kuanzisha uinjilisti bila kujitambulisha kunamfanya aendelee kujiuliza, “Huyu ni nani anayeongea?” badala ya kumfikiria Kristo Yesu na ujumbe wako.

3. Fanya urafiki naye kwa kuongea kuhusu mambo anayopenda yeye kwanza.

Usiingie nyumba na kuanza kumtwanga na Injili mara moja. Chukua muda kupata kumfahamu yule unayeongea naye. Tafuta kujua kwa urafiki jinsi alivyo. Lakini jiangalie usije ukaonekana kama mpelelezi au polisi! Umfurahishe kwa kusifu mambo yake mazuri. Kwa mfano unaweza kusifu watoto, nyumba, mifugo, shamba, picha zilizobandikwa ukutani, n.k. Ukifanya hivyo atapenda kusikiliza ujumbe wako zaidi.

4. Tafuta mwingilio wa kuanzisha Injili kwa njia iliyo na maana kwake.

Katika mambo uliyojifunza juu yake ujitahidi kupata neno la kugeuza mazungumzo yawe juu ya Yesu Kristo na kazi yake. Usitangaze mabadiliko haya, bali uyafanye taratibu ili ionekane kuwa maendeleo ya mazungumzo yako ya kiurafiki. Mwingilio huo utafungua mlango wa kueleza Injili.

5. Ujumbe wako ulenge moyo wake na jinsi alivyo.

Katika mazungumzo yote jaribu kugusa pale anapoumwa kiroho ili aweze kufaidika sana na maana ya wokovu kwake. Usiongee tu mambo ya nje na ya kimwili. Bali weka kiini cha mazungumzo yenu kuwa mambo ya kiroho.
 
 6. Aliye mshiriki mkimya afanye kazi zake.

Kama uliamua kuwa mshiriki mkimya usifikiri huna kazi wakati mwenzako anaeleza Injli. Kazi zako ni za muhimu sana. Lazima ufuate mazungumzo na uwe macho.

a. Mshiriki mkimya ahakikishe kwamba anayeshuhudia anakaa karibu na msikilizaji ili waweze kusikilizana vizuri na kusoma Biblia pamoja bila shida.

b. Mshiriki mkimya aangalie vurugu zo zote ambazo zinaweza kumvuta akili msikilizaji na kumfanya asisikilize ujumbe. Anaweza kujibu maswali ya wengine yasiyohusika, kucheza na watoto, au kuendeleza kazi ambayo msikilizaji alikuwa akifanya kabla hamjaanzisha mazungumzo naye.

c. Yampasa mshiriki mkimya kusikiliza kwa umakini wakati mazungumzo yanaendelea. Maana anaweza kuombwa kusaidia na kuchangia wakati wo wote. Kama hajasikiliza njiani atachanganya mambo tu atakapoombwa kuongea.

d. Vilevile, mshiriki mkimya anapaswa kuomba kimoyo moyo wakati Neno la Mungu linaelezwa.

Kuwa mshiriki mkimya ni njia nzuri kujifunza jinsi ya kushuhudia. Anayejifunza kushuhudia anapaswa kuchukua nafasi kushuhudia kidogo kidogo hadi anaweza kufanya mwenyewe.

7. Mshuhudiaji aulize maswali kuhakikisha kwamba msikilizaji anafuata.

Si vizuri kuongea kama redio bila kukatika. Unapaswa kuongea kwa upole ukisimama mara kwa mara kumwuliza msikilizaji maswali ili uhakikishe unamlenga vizuri na kwamba anafuata na kuelewa yale unayosema.
 
8. Kamwe usibishane.

Mazungumzo yote yawe ya kiurafiki. Msipoelewana usiongeze sauti. Nafuu kuacha ujumbe wa upendo ili mtu akukaribishe siku nyingine kuongea tena kwa kuwa Mungu huweza kuutumia ujumbe wako anapobaki kutafakari. Sijawahi kuona mtu akikata shauri baada ya kubishana. Unaweza kushinda mabishano na kupoteza roho wa mtu.
 
UNAPOMALIZA NA KUACHANA

Jinsi unavyomaliza mazungumzo yenu ni muhimu pia. Kuna mapendekezo machache hapa chini:

1. Ujumlishe mambo makubwa.


Kwa kufanya hivyo unamsaidia kuelewa na kukumbuka yote uliyoyazungumza kwa pamoja. Hii ni muhimu kabla hujaendelea na hatua nyingine.

2. Uhakikishe kwamba ameelewa yote.


Umwulize kama kuna sehemu ya mazungumzo ambayo bado hajaelewa au kama anayo maswali juu ya yale mliyoongea. Angalia usikubali maswali yalio mbali na ujumbe wako. Kama kuna sehemu, urudie polepole ukiongeza maelezo au maandiko zaidi ili upate kumsaidia.

3. Umfanye akate shauri juu ya ujumbe wako.


Ni muhimu sana kumfikisha msikilizaji katika mahali pa kuona ni lazima aamue uamuzi fulani. Injli inahitaji kufanyiwa kazi kwa kuwa siyo hadithi ya kufurahisha tu. Umwoneshe faida ya kumpokea Kristo na jinsi ya kumpokea Kristo. Umwulize kama anataka kuamini au kukataa ujumbe huo.

4. Achana kwa maombi na urafiki.

Atake, asitake kukata shauri, ni nzuri kuomba ruhusa kuongoza kwa maombi ukimshukuru Mungu kwa mazungumzo na kumwombea msikilizaji kulingana na jibu lake. Pia, uachane katika hali ya urafiki. Usimfanye kuwa adui ikiwa hataki kuamini, kwani Roho Mtakatifu anaweza kutumia ulichosema leo kumwongza mbeleni ukiachana kiurafiki.

5. Acha maandiko au kipeperushi na jinsi ya kuwasiliana.


Kwa njia hiyo msikilizaji ataweza kubaki kusoma neno zaidi na kufurahi kwamba ulimpenda hata kumpa zawadi hiyo. Vilevile akiwa na maandiko haya, atajua namna ya kukufuata au kukuita kumsaidia zaidi mbeleni. Isitoshe, maandiko haya yaweza kusomwa na wengine nyumbani mwake pia.

6. Kwa mtu aliyekata shauri ufanye mipango ya kumfuatilia na kumjenga.


Neno hili tutajifunza zaidi katika masomo ya 11 na 12. Kwa sasa, yatosha kusema ni lazima mpango maalum ufanywe na yule aliyeamua kumpokea Kristo kama Mwokozi wake.

Hizi ni sehemu tatu zinazohusu njia au jinsi ya kushuhudia watu mtu kwa mtu na nyumba kwa nyumba. Jitahidi kufuata mapendekezo haya unapoenda kufanya uinjilisti wa mtu kwa mtu na uone kama Mungu atabariki sana kazi yako na kuifanya iwe “uinjilisti ufanyao kazi”.
 
MASWALI NA MAJADILIANO

  1. Kwa nini ni muhimu kuangalia jinsi tunavyoongea na watu tunapowashuhudia?
  2. Kabla hujafika kwa mtu unayemshuhudia ni muhimu uamue jambo gani?
  3. Kazi ya mshiriki mkimya ni nini?
  4. Kamwe usifanye nini? Kwa nini?
  5. Unapoachana na mtu uhakikishe nini?
  6. Kuacha maandiko, jina, na simu namba yako kunasaidia nini?
  7. Kwa nini watu waende na timu ndogo badala ya timu kubwa?

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 7
Proudly powered by Weebly