GMI PUBLICATIONS
GMI PUBLICATIONS
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano
  • Home
  • Kupakua Vitabu
  • Kuhusu Sisi
  • Mawasiliano

UINJILISTI UFANYAO KAZI

- 12 -

Kumfuata na Kumjenga Aliyeamini

Mtoto anapozaliwa duniani tunafurahi sana na kusherehekea. Wakati mwingine tunacheza na kula. Huwa tunawataarifu marafiki na familia nzima. Ingekuwaje ikiwa baada ya kusherehekea, wazazi wangemwacha mtoto peke yake kujitegemea wakiendelea na shughuli za maisha bila kumjali. Tungesema wazazi hawa wamepungukiwa akili! Lakini ajabu ni kwamba katika mambo ya kiroho jambo hilo linatendeka sana! Watu wanakata shauri na kuzaliwa kiroho halafu mwinjilisti anaondoka na kuwaacha bila utunzaji wo wote.

Kwa nini kazi hii ya kuwafuatilia na kuwajenga walioamini inaachwa sana bila kufanyika? Mimi napenda kutoa sababu tano nilizogundua mimi.
 
SABABU ZA KUTOMFUATILIA ALIYEAMINI

1. Hakuna mpango.

Mwinjilisti hakutegemea kwamba mtu angekata shauri na kwa sababu hiyo hakupanga jinsi ya kumfuatilia. Maana amezoea kutupa mbegu tu bila kutazamia mavuno.

2. Kukosa elimu.

Mara nyingine mtu anayeshuhudia hafuatilii waliookoka kwa sababu hajui jinsi ya kuwafuatilia. Hafahamu namna ya kuutunza Mkristo mpya ili asimame imara ndani ya Kristo.

3. Kutojua umuhimu wake.

Wainjilisti wengi wanatambua umuhimu wa kueneza Injili lakini hawajawahi kufikiria kwamba kumwaga mbegu ni mwanzo wa taratibu (process) ndefu. Hawafikiri kuwa wanapaswa kuangalia jinsi ya kumkuza mwongofu. Zaidi hawajaelewa jinsi ilivyo rahisi kwa muumini mpya kuanguka katika imani yake asiposaidiwa.
 
 4. Kukosa uwezo.

Wengine hupenda kushuhudia mbali na nyumbani. Kwa sababu hiyo wakisharudi nyumbani wanakosa uwezo wa kuwafikia wale walioamini tena ili wawasaidie kukua kiroho. Pengine hawana pesa, muda, au hata chombo cha kusafiria ili wawafuatilie tena.

5. Kazi ya ufuatiliaji haina sifa

Unapofanya uinjilisti na watu watatu wanakata shauri, hii ni taarifa nzuri kuwatangazia watu. Kuna hatari kwa wainjilisti kuzoea kushuhudia na kutangaza kanisani idadi ya waliookoka bila kujali malezi yao. Mtu anaweza kusaidia watu 100 kwa mwaka kukata shauri akisifiwa sana kanisani kwa kazi zake wakati asilimia 90 wamemwacha Bwana kwa vile walikosa ufuatiliaji. Anayefanya kazi ya kuwafuatilia waumini wapya siku hadi siku haonekani na hasifiwi kama mwinjilisti huyu. Basi, kwa sababu hiyo, watu huacha kazi ya ufuatiliaji na kukimbilia ile ambayo italeta sifa zaidi. Maana, sisi sote tunapenda kupongezwa kwa kazi zetu.

6. Ni kazi ngumu.

Kazi ya kuwafuata na kuwajenga waumini wapya ni kazi ngumu. Kazi hii inatumia muda mwingi. Matokeo ya kazi hii hayaonekani haraka kama kazi zingine. Isitoshe muumini mpya anaweza kufuatiliwa sana na mwisho aamue kutoendelea katika imani yake. Hapo ndipo kazi ya mlezi inakuwa ngumu zaidi.
 
UMUHIMU WA KUFUATILIA ALIYEAMINI

Tunaweza kuangalia Maandiko Matakatifu kugundua umuhimu wa kazi hii machoni pa Mungu.

3 Yohana 4 - “Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli.”

1 Yohana 2:28; 2 Yohana 8 - “Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake katika kuja kwake. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu.”
 
1 Petro 5:2 - “Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.”

Yohana 21:16 B “Akamwambia tena mara ya pili, ‘Simoni wa Yohana, wanipenda?’ Akamwambia, ‘Ndiyo Bwana wewe wajua kuwa nakupenda.’ Akamwambia, ‘Chunga kondoo zangu.’”
 
USHAURI KATIKA KUMFUATILIA ALIYEAMINI

Ufuatiliaji unalenga kumfanya muumini mpya akue kiroho na asimame imara katika uhusiano wake na Mungu. Zaidi ufuatiliaji unamsaidia huyu aliyeamini kushirikishwa kikamilifu kanisani na kuanza kufanya huduma za Mungu, hata kuleta wengine kwa Kristo. Kazi ya uinjilisti isiyo na shabaha hizo inastahili kupangwa upya. Hapo chini ni mambo machache yaliyo muhimu zaidi kwa muumini mpya. Kuna mambo mengine mengi kuliko hayo tu ambayo muumini mpya anapaswa kuyapata ili akomae kiroho. Lakini mambo haya ni yale ya kuanza nayo.

  1. Umfundishe kuhusu kuzaliwa mara ya pili na jinsi gani mtu hupata kuzaliwa na Mungu na kuwa Mkristo.
  2. Umfundishe jinsi ya kusali (kuomba) kila siku ili awe na mawasiliano na Baba yake wa mbinguni.
  3. Umfundishe jinsi na umuhimu wa kusoma Biblia kila siku ili apate chakula cha kiroho.
  4. Umfundishe umuhimu wa kuabudu na kushirikiana katika jamii mpya, yaani, kanisa.
  5. Umfundishe na kumsaidia kufahamu jinsi ya kushinda dhambi na tabia mbaya siku hadi siku.
  6. Umfundishe jinsi ya kuwashuhudia wengine imani yake kwa uhakika.
  7. Umfundishe zaidi kuhusu uhakika wa wokovu wake na usalama wa milele wa wokovu wake.
  
MASWALI NA MAJADILIANO

  1. Kwa nini watu wengi hawafanyi kazi ya kuwafuatilia na kuwajenga waumini wapya?
  2. Kati ya sababu zilizotolewa, ni ipi ambayo unafikiri ni sababu kuu?
  3. Kuna sababu nyingine zinazozuia ufuatiliaji? Zitaje.
  4. Kwa nini ni muhimu kuwafuatilia na kuwajenga waumini wapya?
  5. Shabaha kuu za uinjilisti ni nini?
  6. Unapaswa kumfundisha muumini mpya mambo gani?

RUDI KWENYE ORODHA YA SURA
sura ya 13
Proudly powered by Weebly